Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO Tanzania yazindua tawi la Mtandao wa Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi TAWFA

Mtandao wa Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania
UN News
Mtandao wa Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania

FAO Tanzania yazindua tawi la Mtandao wa Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi TAWFA

Ukuaji wa Kiuchumi

Katika kutekeleza lengo namba 8 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kuhusu ajira za staha na ukuaji kiuchumi sambamba na namba 5 la usawa wa kijinsia, shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo duniani FAO nchini Tanzania,  limezindua tawi la tatu la Mtandao wa Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi TAWFA kupitia mradi wake wa kukuza mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi katika ziwa Tanganyika.

Sherehe za uzinduzi huo zimefanyika mkoani Kigoma nchini humo ambapo wanawake wavuvi, viongozi wa serikali na wafanyakazi wa FAO walifungua rasmi tawi hili ikiwa ni la tatu nchini humo baada ya mwengine mawili yaliyozinduliwa huko kanda ya Ziwa Victoria na Ukanda wa Bahari ya Hindi.

Uzinduzi huo unafanyika kupitia mradi wa FISH4ACP unaotekelezwa katika mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ambapo Mratibu wa Sekta ya Uvuvi Kitaifa kutoka FAO, Oliva Mkumbo akizungumza na Devotha Songorwa wa Redio washirika wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa alimueleza lengo ni kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia uvuvi ili kuinua kipato cha familia na kuondokana na umasikini.

“Lengo la kuanzisha jukwaa la wanawake ni kuwawezesha kina mama ili mchango wao utambulike na kuleta athari chanya katika jamii. Tunataka kila mwanamke anayejihusisha na mnyororo wa thamani katika uvuvi anakuwa na sehemu ya kutoa mawazo yake na kubadilishana uzoefu ili kwa pamoja wachangie uboreshaji wa uvuvi,” Anasema Oliva.

Oliva Mkumbo Mratibu wa Sekta ya Uvuvi Kitaifa kutoka FAO
UN News
Oliva Mkumbo Mratibu wa Sekta ya Uvuvi Kitaifa kutoka FAO

Mratibu huyo wa FAO amesema hili halitakuwa tawi la mwisho nchini humo. “Jukwaa rasmi kitaifa lilifunguliwa 2017 ili kuwafikia wanawake wengi wakaanzisha Zone Chapters, Chapter ya Kanda ya Ziwa Victoria 2019, baadaye ikaja ya Uvuvi baharini, Kanda ya Ziwa Tanganyika na baadaye huko tutakuwa na linguine linalohusika na wavuvi kutoka katika maziwa madogo madogo,” Ameeleza Mratibu huyo.

Beatrice Mmbaga ni Mwenyekiti wa Taifa wa Mtandao wa Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA) anasema jukwaa hili ni sehemu ya kutatua changamoto zinazowakabili kina mama walio katika sekta ya uvuvi.

“Nia ya kuanzisha chombo hiki ni kumfikia mama popote alipo anayejishusisha na samaki na mazao yake Tanzania nzima ndipo sasa tunashuka ngazi za chini katika Mikoa yetu, Kanda na Wilaya ili tuwe na sauti moja kwa sababu kina mama ndiyo asilimia kubwa wanajihusisha na samaki baada ya mavuvi hasa kwenye kuchakata na masoko lakini wana changamoto nyingi sana,” amebainisha Mwenyekiti huyo.

Wanawake wajasiriamali katika sekta ya Uvuvi Tanzania
UN News
Wanawake wajasiriamali katika sekta ya Uvuvi Tanzania

Kwa upande Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia masuala ya Udhibiti Ubora na Mazao ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Steven Lukanga amebainisha kwamba wanawake bado wanahitajika kupatiwa elimu ya uvuvi salama na kukidhi mahitaji ya walaji.

“Kikubwa ni kuwajengea uwezo wanawake kutambua viwango vinavyopaswa kuzalisha yale mazao yanayowaendea walaji kwa kuzingatia viwango vilivyopo chini ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwahiyo sisi kama wizara tunashirikiana nao kuhakikisha wachakataji wanawake wanakidhi viwango vinavyotakiwa,”Amesema Lukinga.