Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FISH4ACP yainua wavuvi wake kwa waume ziwa Tanganyika

Mfanyakazi akipakua shehena ya samaki
FAO
Mfanyakazi akipakua shehena ya samaki

FISH4ACP yainua wavuvi wake kwa waume ziwa Tanganyika

Ukuaji wa Kiuchumi

Mradi wa FISH4ACP unaotekelezwa na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kwa ubia na Muungano wa Afrika na ule wan chi za Karibea na Pasifiki, kwa ufadhili kutoka Muungano wa Ulaya na serikali ya Ujerumani, umeleta matumaini na mafanikio kwa wavuvi wa ziwa Tanganyika mkoani Kigoma nchini Tanzania kufuatia mafunzo waliyopatiwa wavuvi hao.

Kutana na Zena Masoud, mjasiriamali wa samaki katika Ziwa Tanganyika nchini Tanzania mmoja wa wanufaika wa mradi wa FISH4ACP. Zena anasema,“Nachakata dagaa, nanunua dagaa wabichi nawaanika, wakikauka naenda kuwauza sokoni. Maisha na biashara hii ya samaki si mabaya kwa sababu tumejenga nyumba na sasa hivi nasomesha watoto.” 

Mradi wa FISH4ACP unalenga kuongeza mnyororo wa thamani wa dagaa na samaki wengine kama vile migebuka kwenye Ziwa Tangayika. 

Bahati Migezo naye huchakata mazao ya uvuvi kulingana na mahitaji ya mteja wake na anasema,“Ninapofika eneo la uvuvi kuna kanuni bora ya kuzingatia ili kukabili ushindani, nayo ni kupata bidhaa bora. Bidhaa iliyo bora kidogo huwa ni adimu. Kwa kuwa hatujaweza kuwa na vitendea kazi vya kukidhi ubora kwa asilimia 100, hivyo tunalazimika kufanya uchaguzi wa hali ya juu ya bidhaa inayoweza kukidhi mahitaji ya soko. “ 

Pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo, mafunzo kupitia FISH4ACP yamekuwa muarobaini. “Mafunzo liyopata kwa awamu yanasaidia kuboresha bidhaa zetu ambapo hata sasa kuna watu wanakubali bidhaa hizo nje ya nchi. Najua FISH4ACP inaweza kutusaidia na nina matumaini ya kuboresha maisha na kukidhi mahitaji ya masoko ambayo tumekuwa tunashindwa kukidhi.” 

Na kwa Zena, ombi maalum kwa FAO na wadau wa mradi huo ni,  “Kama tutapata vyombo vizuri vya uvuvi, itakuwa bora kwa sababu ukiwa na vyombo vizuri una uhakika wa mazao mazuri kutoka Ziwani. Na vile vle tunaomba viwanda wakati huu wa masika, kama tuna miundombinu mizuri tungeanika vizuri lakini sasa mvua zikinyesha dagaa zinaharibika.” 

Baada ya ombi, Zena akatoa shukrani zake. "Tunafurahia sana mradi huu, tunaishukuru serikali kwa kutuletea mradi huu, na tulikuwa tunaomba kama kuna mikopo serikali itusaidie hata kwa wavuvi pia. Kuna kipindi mtu anashindwa kufanya biashara kwa sababu hana mtaji.”