COVID-19 ni msumari wa moto juu ya kidonda kwa watoto DRC:UNICEF 

31 Machi 2020

Mfumo wa afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, unahitaji msaada wa haraka wakati huu ukilemewa na magonjwa ya surau na kipindupindu yanayokatili maisha ya maelfu ya watoto pamoja na tishio la janga jipya la virusi vya Corona COVID-19.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, ambayo inasema juhudi za kukabiliana na Ebola Mashariki mwa nchi hiyo zimebadili mtazamo na kupeleka rasilimali katika janga hilo kutoka kwenye vituo vingine vya afya ambavyo tayari vimezidiwa kwa kukabiliana na magonjwa mengi ya mlipuko.

Kituo cha afya cha wilaya ya Nsele Congo DRC kikitoa huduma za vipimo kwa watoto na matibabu ya surua
©UNICEF/Patrick Brown
Kituo cha afya cha wilaya ya Nsele Congo DRC kikitoa huduma za vipimo kwa watoto na matibabu ya surua

Tangu mwanzo wa mwaka 2019 mlipuko wa surau ambao ni mbaya zaidi kushuhudiwa duniani umekatili maisha ya watoto zaidi ya 5,300 wenye umri wa chini ya miaka mitano huku pia kukiwa na wagonjwa 31,000 wa kipindupindu.

Kana kwamba maradhi hayo hayatoshi ripoti inasema "sasa mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 unasambaa kwa kasi na kutoa mtihani mkubwa kwa nchi hiyo ambayo imeelezwa kuwa katika hatari zaidi barani Afrika.”

UNICEF imeongeza kuwa hali hii ni sawa na kuweka msumari wa moto juu ya kidonda kwani katika vituo vya afya vya umma, vifaa, wahudumu wenye ujuzi na fedha ni haba. Vituo vingi vinakosa hata huduma za msingi za maji na usafi na kiwango cha chanjo ambacho kilikuwa chini sasa kimeshuka zaidi kwa mwaka mmoja uliopita.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNICEF takriban watoto milioni 3.3 nchini DRC wanakosa huduma za msingi za afya, huku katika nchi nzima watoto milioni 9.1 karibu mtoto 1 kati ya 5 waliochini ya miaka 18 anahitaji msaada wa kibinadamu.

UNICEF imeonya kwamba "endapo vituo vya afya havitapata njia ya kufikisha chanjo, lishe na huduma zingine za msingi ikiwemo kwenye maeneo ya vijijini nchini humo basi tuna hatari ya kushuhudia maisha na mustakabali wa watoto wengi wa Congo ukisambaratishwa na magonjwa yanayoweza kuzuilika."

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter