Watoto 4500 wamepoteza maisha kutokana na surua DRC:UNICEF

27 Novemba 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetaka mkazo utolewe pia kukabiliana na ugonjwa wa surua ambao linasema unaua idadi kubwa ya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kuliko hata Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. 

Kupitia tarifa yake iliyotolewa leo mjini Kinshasa mwakilishi wa UNICEF nchini DRC Edouard Beigbeder amesema “tangu kuanza kwa mwaka huu watu zaidi ya 5000 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa wa surua huku zaidi ya asilimia 90 ya watu hao ni watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.”

Ameongeza kuwa wakati mlipuko wa ebola ambao hadi sasa umeshakatili maisha ya watu zaidi ya 2000 huko Mashariki mwa DRC umepewa uzito mkubwa wa kimataifa , ugonjwa wa surua umekatili maisha ya mara mbili zaidi ya ebola na unaendelea kutopewa uzito mkubwa.

Amesema “machafuko na kutokuwepo kwa usalama, ukosefu wa fursa za kupata huduma za afya na upungufu wa chanjo na vifaa tiba katika maeneo yaliyoathirika zaidi inamaanisha kwamba maelfu ya wa watoto wanakosa kupewa chanjo muhimu wanazostahili ambapo matokeo yake ni kupoteza maisha.”

Ametaja sababu zingine zinazofanya Watoto kukosa chanjo ikiwa ni pamoja na imani, mila na utamaduni lakini pia matumizi ya mitishamba.

Bwana Beigbeder amesisitiza kuwa “licha ya changamoto nyingi tuna nyezo na elimu ya kuzuia surua kwa kutumia chanjo ambazo ni salama , za gharama nafuu na zinazofanyakazi . Cha msingi ni kumfikia kila mtoto bila kujali wapi aliko.”

Hivi sasa amesema UNICEF na wadau wanaendelea kuendesha kampeni ya chanjo ya surua katika maeneo yaliyoathirika zaidi na kufikisha vifaa kwenye vituo vya afya pamoja na madawa ya kutibu walio na dalili za ugonjwa huo.

Hadi sasa UNICEF imeshasambaza vifaa 1317 vya kukabiliana na surua vikujumuisha dawa za viuavijasumu, maji ya kuongeza nguvu, matiné ya vitamina A na dawa zingine muhimu zinazohitajika.

Hata hivyo shirika hilo limesema “hizo zinaweza kuwa ni suluhu za muda mfupi kinachohitajika ni uwekezaji katika kuimarisha programu ya kitaifa ya kampeni ya chanjo  na kuimarisha mfumo wa afya vitu ambavyo ni muhimu sana katika kuhakikisha afya na mustakabali bora wa watoto wa taifa hilo.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud