Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu zaidi ya 40 wapoteza maisha na nyumba zaidi ya 32,000 kuharibiwa na mafuriko DRC:OCHA/UNICEF

Watoto nchini Jamhuri ya kidemkrasia ya Congo,DRC
© UNICEF/Vincent Tremeau
Watoto nchini Jamhuri ya kidemkrasia ya Congo,DRC

Watu zaidi ya 40 wapoteza maisha na nyumba zaidi ya 32,000 kuharibiwa na mafuriko DRC:OCHA/UNICEF

Tabianchi na mazingira

Mafuriko mabaya zaidi katika kipindi cha miaka 25 yalikumba eneo la Ubangi Kaskazini na Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, mafuriko hayo yamesababisha hasara na uharibifu mkubwa ikiwemo  kupoteza maisha ya zaidi ya watu 40, nyumba zaidi ya 32,000 vyanzo vya maji 632 na shule na vituo vya afya 142.

Tathimini ya awali inaonyesha kuwa watu zaidi ya 400,000 wameathirika na mafuriko hayo hasa katika eneo la mto Ubangi Kaskazini Magharibi wa DRC hasa katika majimbo ya Kaskazini na Kusini mwa Ubangi yanayopakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, lakini pia mafuriko yameripotiwa katika majimbo ya Maniema, Tshopo na Haut-Uele kufuatia mvua kubwa zilizoanza kunyesha tangu mwezi Oktoba.

Mahitaji ya dharura

Watu zaidi ya 40 walipoteza maisha mapema wiki hii kufuatia mvua kubwa na maporomoko ya udongo yaliyotokea katika mji mkuu wa DRC Kinshasa na kusababisha mafuriko makubwa katika viunga vya mji huo.

OCHA inasema vituo vya maji na vyoo vimeharibiwa na fursa ya watu kupata maji safi na salama na huduma za usafi ni ndogo sana na hatari kubwa ya magonjwa yatokanayo na maji hususan kipindupindu inaongezeka kutokana na kufurika kwa vyoo na mazingira machafu.

Kwa kupitia msaada wa dharura shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF , limepeleka msaada wa kwanza wa dharura ukiwa na maji, vifaa vya usafi na vya afya kwa njia ya ndege hadi kwa washirika wao kwenye maeneo ya Zongo na Libenge ambako ndio kitovu cha janga hili la kibinadamu kwenye jimbo la Ubangi Kusini. 

OCHA pia imepeleka wafanyakazi wake katika majimbo yote yaliyoathirika ili kusaidia kuratibu huduma za misaada. Pia tathimini inafanyika hivi sasa nchi nzima ili kubaini ni jumla ya watu wangapi walioathirika na wanaohitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.

Mpango wa msaada umeanzishwa na serikali kwa msaada wa Umoja wa Mataifa na washirika wengine ambao utasaidia kutoa kipaumbele cha masuala ya muhimu kama malazi, maji na usafi, na vifaa ambavyo si chakula kuwasaidia wale walioathirika zaidi.

Duru ya pili ya msaada wa dharura itapelekwa hivi karibuni ikijumuisha pia wataalam wa maji na masuala ya usafi katika majimbo yaliyoathirika zaidi.

Mbali ya mafuriko na Ebola

Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya OCHA na UNICEF yanasema mbali ya mafuriko haya na ugonjwa wa Ebola ambao unaendelea , hadi kufikia tarehe 10 novemba mwaka huu kumekuwa na visa 25, 818 vya ugonjwa wa kipindupindu ikiwemo vifo 457.

Pia kuna mlipuko wa surua nchi nzima ambao umeelezewa kuwa ni mlipuko mkubwa zaidi duniani na unaosambaa haraka ambao tayari umeshakatili maisha ya watu zaidi ya 5000 na asilimia zaidi ya 90 ya waliopoteza maisha ni watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.