Tunahofia raia, ghasia zinavyoshika kasi mashariki mwa DRC:UNHCR

29 Novemba 2019

Shirika la Umoja wa mataifa lakuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linatiwa wasiwasi mkubwa kuhusu maisha ya raia wakiwemo wakimbizi wa ndani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambako machafuko yanazidi kushika kasi.

Takribani watu 100 wameuawa kwenye jimbo la Beni tangu kuanza kwa operesheni za serikali za kukabiliana na wapiganaji wa kiundi la ADF 30 Oktoba mwaka huu.

UNHCR inasema mamia ya watu ambao wamekuwa wakikimbia mashambulizi na mapigano baina ya jeshi la serikali na ADF wamekuwa wakipata hifadhi kwenye mji wa Beni ambako usalama mdogo na maandamano makubwa yaliyofanyika mapema wiki hii yamesababisha kukatwa kwa huduma za misaada ya kibinadamu.

Duru zinasema shambulio la karibuni katika Kijiji nje ya mji wa Beni liliua watu 19 siku ya Jumatano wiki hii na wafanyakazi wanne wa huduma za Ebola kuripotiwa kuuawa pia siku hiyo hiyo jioni kwenye kambi ya wafanyakazi wa huduma ya Ebola mjini Biakato kwenye ofisi ya kuratibu huduma za Ebola ya Mangina.

Leo shirika la UNHCR limetoa wito wa kurejesha usalama haraka kwenye jimbo la Beni ili mashirika ya misaada ya kibinadamu yaweze kuwasaidia watu walioathirika zaidi jimboni Beni ikiwemo mamia ya familia ambazo kwa sasa zinalala makanisani na mashuleni kwa kuhofia usalama wao.

UNHCR inasema “watoto ndio wanaohitaji msaada wa haraka wengi wao wakiwa wamepoteza wazazi wao wote au wamewasili bila kuwa na mtu yeyote. Na hii ni tishio kubwa kutokana na makundi yenye silaha yanayoingiza watoto jeshini .”

Pia shirika hilo limesema waathirika wengine wakubwa ni wanawake ambao wanakabiliwa na ukatili wa kingono, manyanyaso na hatari ya dhuluma. “Tunahofia Maisha mengi Zaidi ya watu yatapotea endapo huduma za kibinadamu na utulivu havitorejea haraka kwenye eneo hilo” limesema shirika hilo.

Wafanyakazi wa UNHCR wamepelekwa kwenye eneo hilo la Beni wanaohusikana masuala ya ulinzi, malazi na uratibu. Hivi sasa wanajenga malazi ya dharura kwa watu waliotawanywa, kudumisha amani miongoni mwa wakimbizi wa ndani na jamii zinazowahifadhi na kushirikiana na mamlaka za kijamii kukusanya taarifa kuhusu wakimbizi wa ndani, kuwaorodhesha walio katika hatari zaidi ilikuweza kuwasaidia kwa urahisi.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi mji wa Beni ni maskani ya takribani wamu 500,000 na miongoni mwao 275,000 ni waliotawanywa na machafuko au wakimbizi wa ndani. 

Na kutokana na kuendelea kwa hali mbaya ya usalama wengi wamejikuta wamekwama katikati ya makundi ya wapiganaji.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter