Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde DRC sitisheni uhasama na kuwawajibisha wauaji wa raia:Guterres

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akisalimia wakazi wa Beni wakati wa doria huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
UN Photo/Sylvain Liechti
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akisalimia wakazi wa Beni wakati wa doria huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Chonde chonde DRC sitisheni uhasama na kuwawajibisha wauaji wa raia:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Antonio Guterres amerejea wito wake wa kusitisha uhasama kimataifa na kuyataka makundi yote yenye silaha kuweka silaha hizo chini na kujiunga katika mchakato wa amani, baada ya raia zaidi ya 20 kuuawa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Akisistizan umuhimu wa serikali ya DRC kuchukua hatua Madhubuti kushughulikia vyanzo vya mizozo Mashariki mwa nchi hiyo Katibu Mkuu amesema raia wasio na hatia hupoteza maisha kila uchao vita vinapoendelea. 

Kwa mujibu wa duru za Habari mwanzoni mwa wiki hii raia zaidi ya 20 waliuawa katika shambulio linalodaiwa kufanywa na waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) kwenye vijiji vya Tingwe, Mwenda na Nzenga karibu na mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC. 

Bwana. Guterres amelaani vikali machafuko na mauaji hayo dhidi ya raia na kutoa wito kwa wahusika wote kusakwa, kukamatwa na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.  

Pia kufuatia mauaji hayo ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na serikali ya DRC, huku akiahidi kwamba Umoja wa Mataifa kupitia mpango wake nchini humo MONUSCO, utaendelea kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha ulinzi wa raia kwa kuzingatia majukumu yake na pia kusaidia juhudi za kitaifa za kuleta amani na utulivu wa kudumu nchini humo. 

Eneo la Mashariki mwa DRC mara kwa mara limekuwa likilengwa na mashambulizi ya waasi na vikundi vyenye silaha na mara zote waathirika wakubwa huwa ni raia hususani wanawake na watoto.