Watu zaidi ya 100,000 wafurushwa na mapigano mapya Kivu Kaskazini:UNHCR

3 Mei 2019

Hali ya kutokuwepo na usalama na machafuko mapya katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, imelazimisha watu zaidi ya Laki Moja kufungasha virago na kuzikimbia nyumba zao mwezi April kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

 

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi, msemaji wa UNHCR Babar Baloch amesema wakati mashambulizi yakiendelea kuwatia wasiwasi raia hofu kubwa ya shirika hilo ni kuhusu usalama wa raia hao.

Hivi sasa wakimbizi wa ndani wako katika hali mbaya na jitihada za kuwafikia kwa ajili ya mahitaji muhimu zinakabiliwa na kikwazo kutokana na hali tete ya usalama.Baloch ameongeza kwamba "iankadiriwa kwamba hadi watu 60,000 wamekimbia Aprili kutokana na mapigano eneo la Kamango Karibu na mji wa Beni. Na mwezi huohuo takriban watu 50,000 walikimbia kwenye maeneo ya Lubero ambako jeshi la DRC lilikuwa linapigana na makundi yenye silaha ya Mai Mai.”

Na wakati mfululizo wa mashambulizi kutoka kwa makundi yenye silaha ndani ya mji wa Beni yamesita, Baloch amesema sasa yamehamia katika maeneo ya vijijini.

Utekaji nyara na mauaji vimeaathiri kwa kiasi kikubwa watu, na mara nyingi waliotawanywa ndio walengwa wakubwa, na kwamba,“wiki iliyopita maiti watano walioharibika walipatikana kwenye eneo la masisi takribani kilometa 60 Kaskazini Magharibi mwa Goma. Maiti hao ni pamoja na tatu za watoto. Watu wanne kati ya waliokufa walikuwa wametekwa kutoka Kasunga, karibu na makazi ya watu waliotawanywa.”

Ameongeza katika eneo hilohilo zaidi ya wakimbizi wapya wa ndani 20,000 wamewasili katika miezi mitatu iliyopita kwenye miji mitatu midogo  ya Mweso, Kashuga na Kirumbu eneo la  Masisi.

Timu ya UNHCR iliyozuru eneo hilo imepokea taarifa za ubakaji na makundi yenye silaha kuingiza watoto vitani.

Jimbo la Kivu ya Kaskazini kwa mujibu wa shirika hilo linasalia kuwa moja ya lililoathirika sana na wakimbizi wa ndani ambao sasa ni zaidi ya milioni moja, lakini pia ndilo lenye idadi kubwa ya visa vya ukatili wa kingono na ukatili wa kijinsia nchini DRC.

Hofu ya UNHCR ni kwamba ombi lake la dola milioni 47 zinazohitajika kwa mwaka huu 2019 kwa ajili ya wakimbizi wa ndani DRC hadi sasa shirika hilo limepokea dola milioni 6.2 pekee.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud