Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu wa kina mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP24

Kutoka katika mtumbwi, kijana akitizama mto karibu na Sirajganj Bangladesh,eneo ambalo limeathirika na mmomonyoko uliowaacha wengi bila makazi.
IOM/Amanda Nero
Kutoka katika mtumbwi, kijana akitizama mto karibu na Sirajganj Bangladesh,eneo ambalo limeathirika na mmomonyoko uliowaacha wengi bila makazi.

Fahamu wa kina mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP24

Tabianchi na mazingira

Wakati kiwango cha joto kikiendelea kupanda duniani , hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi zinazorota na fursa ya kulishinda jinamizi hili inaendelea kuwa finyu. Jumapili wiki hii Umoja wa Mataifa utaanza majadiliano muhimu ya jinsi gani ya kushughulikia tatizo hilo kwa pamoja na kwa haraka, katika wiki mbili za mkutano wa 24 wa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP 24 utakaofanyika mjini Katowice nchini Poland.

Maelfu ya viongozi wa dunia, wataalam, wanaharakati, wabunifu, sekta binafsi na wawakilishi kutoka asasi za kiraia na jumuiya za wenyeji watakusanyika ili kushughulikia mpango wa hatua za pamoja kwa minajili ya kutimiza ahadi muhimu iliyowekwa na nchi zote mjini Paris, Ufaransa miaka mitatu iliyopita

Idhaa ya Umoja wa  Mataifa imeandaa muongozo wa kuelekea COP24 ili kujibu baadhi ya maswali makubwa ambayo unaweza kuwa nayo kuhusu mpango huo wa hatua za pamoja.

Msingi wake: UNFCCC, UNEP, WMO, IPCC, COP 24, Mkataba wa Kyoto, Mkataba wa Paris. Je vyote hivi ni nini? 

Tuvalu, moja ya visiwa vya Bahari ya Pacific vikiwa kwa wastani chini ya mita mbili juu ya usawa wa bahari. Hali hii imetokana na mabadiliko ya tabia nchi.

 Vifupisho hivi na majina haya ya maeneo yanawakilisha nyenzo za kimataifa na mikakati ambayo chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa ilianzishwa ili kusaidia kusongesha mbele hatua za kimataifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Vyote vina jukumu muhimu katika kutuongoza sote kufikia malengo ya kuwa na mazingira endelevu na kwa jinsi gani basi inavyokuwa hatua ya pamoja:

Mwaka 1992, Umoja wa Mataifa uliandaa mkutano mkubwa mjini Rio de Janeiro ulioitwa Earth Summit, ambako mkakati wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi (UNFCCC) ulipitishwa.

Katika mkataba huu Mataifa yaliafikiana "kudhibiti kiwango cha gesi ya viwandani hewani” ili kuzuia kuingilia katika shughuli za binadamu kwenye mfumo wa hali ya hewa. Leo hii mkataba huo umeridhiwa na Mataifa 197. Kila mwaka tangu mkataba huo uanze kutekelezwa mwaka 1994 “mkutano wa nchi wadau yaani COP unafanyika kujadili jinsi gani ya kusonga mbele na tangu hapo kumekuwa na mikutano 23 ya COP na mwaka huu kutakuwa na mkutano wa 24 au COP 24”

Kwa sababu mkataba wa UNFCCC hauna kiwango maalumu cha udhibiti wa utoaji wa gesi ya viwandani kwa nchi na hakuna mfumo wa kuwasukuma , nyongeza kadhaa za mkutaba huo zimejadiliwa wakati wa mikutano ya COP, ikiwemo mkataba mashuhuri wa Kyoto mwaka 1997, ambao ulielezea kiwango cha ukomo wa utoaji gesi chafuzi kwa Mataifa yaliyoendelea kufikiwa ifikapo mwaka 2012 na mkataba wa Paris ukapitishwa mwaka 2015, ambako mataifa yote duniani yaliafikiana kuchukua hatua za kudhibiti kiwango cha ongezeko la joto duniani kusalia nyunzi joto 1.5°C juu ya ilivyokuwa kabla ya maendeleo ya viwanda duniani na kuongeza ufadhili wa kifedha kwenye hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mashirika mawili yanaunga mkono kazi za kisayansi za Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi: Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira (UNEP) na shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani (WMO). Kwa pamoja yaliunda jopo la kimataifa la mabadiliko ya tabianchi (IPCC) mwaka 1988, ambalo linajumuisha mamia ya wataalam maalumu waliotengwa kutoa ushahidi unaoaminika wa kisayansi , kutathimini takwimu na kutoa ushahidi wa kisayansi unaoaminika kwa ajili ya majadiliano ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yakiwemo yanayokuja ya mjini Katowice.

2. Umoja wa Mataifa unaonekna kuwa na mikutano mingi kuhusu mada hii. Je kuna wowote unaozaa matunda?

 

Vijana waliohudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Bonn Ujerumani wakiwa wamebeba kitambaa kilichoandikwa iokoe dunia. Mkutano huo ulihusu mabadiliko ya tabia nchini.

 Mikutano hii imekuwa muhimu sana katika kusaka muafaka wa kimataifa kwenye suala ambalo linahitaji suluhu ya kimataifa. Ingawa hatua zimekuwa taratibu kuliko ilivyopaswa , lakini  mchakato ambao umeghubikwa na changamoto nyingi kama ilivyo malengo yake umesaidia kuzileta nchi pamoja katika mazingira tofauti. Na hatua zimekuwa zikipigwa katika kila kipengele cha safari hii .

Baadhi ya hatua muhimu zilizopigwa hadi sasa zinathibitisha kitu kimoja : Kwamba hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni nzuri na zinaweza kusaidia kuzuia zahma kubwa.

Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa:

- Takribani mchi 57 zimeweza kupunguza kiwango chake cha gesi ya viwandani kwa kiwango kinachohitajika kimataifa kukabiliana na ongezeko la joto duniani.

-Kuna takribani Miradi 51 gharama za hewa ukaa inayofanya kazi ambayo inawatoza wanaotoa hewa chafuzi ya ukaa kwa kila tani.

-Mwaka 2015 nchi 18 za kipato cha juu ziliahidi kuchangia dola bilioni 100 kila mwaka kwa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi katika Mataifa yanayoendelea. Hadi sasa fedha zilizokusanywa ni dola bilioni 70.

3. Kwa nini kila mtu anazungumzia mkataba wa Paris?

Mkataba wa Paris ambao unaipa dunia chaguo pekee la kushughulikia mabadiliko ya tabianchi umeridhiwa na mataifa184,na ulianza kutekelezwa rasmi Novemba 2016

Ahadi zilizo katika mkataba huo ni muhimu sana:

- Kudhibiti kiwango cha ongezeko la joto duniani kusalia chini ya nyuzi joto 2°C na kusaka juhudi za kudhibiti kupanda kwa kiwango cha joto kuwa nyuzi joto 1.5°C.

- Kukusanya fedha kwa ajili ya hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo lengo la dola bilioni 100 kila mwaka kutoka kwa nchi wahisani kwenda kwa nchi za kipato cha chini.

- Kuanzisha mikakati ya kitaifa ya mabadiliko ya tabianchi ifikapo 2020, ikiwa ni pamoja na malengo binafsi waliyodhamiria kuyafikia.

- Kulinda mazingira ambayo yanafyonza hewa ukaa kutoka viwandani ikiwemo misitu .

- Kuimarisha mnepo na kupunguza hatari itokanayo na mabadiliko ya tabianchi.

- Kukamilisha mipango ya makubaliano ya utekelezaji kabla ya kumalizika kwa mwaka 2018.

Marekani ambayo ilijiunga na mkataba huo mwaka 2016, mwezi Julai 2017 ilitangaza nia yake ya kujiengua kwenye mkataba huo. Hata hivyo taifa hilo linasalia kama sehemu ya makubaliano ya mkataba hadi mwezi Novemba 2020 ambapo kisheria taifa hilo linaweza kujiengua.

4. Kwa nini nyuzi joto +1.5°C ni muhimu sana?

Barafu ikiyeyuka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi. Hali hii inaweza kuongeza kina cha bahari.

Kwa mujibu wa  utafiti wa kisayansi uliofanyiwa tathimini na IPCC, kuhakikisha ongezeko la joto duniani halizidi wastani wa nyuzi joto 1.5°C kimataifa kutasaidia kuepuka athari za kudumua kwa dunia na watu wake ikiwa ni pamoja na upotevu wa makazi ambao hautoweza kubadilishwa  kwa wanyama kwenye maeneo ya Arctic na Antactica  ambako mara nyingi kunazuka matukio yenye athari mbaya inayopoteza maisha ya viumbe kama joto la kupindukia, upungufu wa maji ambao unaweza kuathiri zaidi ya watu milioni 300, kutoweka kwa matumbawe ambayo ni muhimu sana kwa majii na maisha ya viumbe vya baharini , kupanda kwa kina cha bahari ambako kunatishia mustakabali wa mataifa ya visiwa vidogo vinavyoendelea na n.k.

Pamoja na yote Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa chini ya watu milioni 420 wanaweza kuathirika na mabadiliko ya tabianchi endapo tutaweza kudhibiti ongezeko la joto duniani likasalia katika kiwango cha nyuzi joto 1.5°C  badala ya nyuzi joto 2°C.

Bado dunia iko mbali katika kubadili mfumo na kuingia kwenye usiozalisha hewa ukaa nyingi na dhamira ya kusonga mbele kufikia huo ni kubwa hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote.

Takwimu zinaonyesha kwamba bado inawezekana kudhibiti mabadiliko ya tabianchi kuwa katika nyuzi joto 1.5°C lakini fursa ya kufanya hivyo inazidi kuwa finyu na itahitaji mabadiliko makubwa katika kila nyanja ya jamii kutimiza hilo.

5. Kwa nini COP 24 ni muhimu ?

 

Salaheddine Mezouar ambaye ni rais wa COP22 na pia Waziri wa Mambo ya nje wa Morocco, (kushoto) akiwa na Rais wa COP21 ambaye pia ni Waziri wa Mazingira wa Ufaransa Ségolène Royal wakati wa ufunguzi wa mkutano wa COP22 Morocco

Mkutano wa mwaka huu wa COP mjini Katowice, Poland, ni muhimu sana kwasababu mwaka 2018 ndio ukomo ambao uliafikiwa na waliotia saini mkataba wa Paris is ili kupitisha mpango kazi wa utekelezaji wa ahadi za mkataba huo. Na hili linajitahi kiungo kimoja cha muhimu sana :” Imani miongoni mwa nchi zote.”

Miongoni mwa vipengele ambavyo vinahitaji kutiliwa mkazo ni ufadhili wa kifedha kwa ajili ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kote duniani. Kwa sababu saa hazigandi katika kukabili mabadiliko ya tabianchi, dunia haiwezi kumudu kupoteza muda zaidi , ni lazima tukubaliane kwa pamoja kuhusu mwelekeo ambao ni madhubuti, wa pamoja, wenye malengo na wa uwajibikaji katika kusonga mbele.

 

 

6.Ushahidi gani utatumika kwa majadiliano kwenye COP 24?

                                                                                                       

Nchi kama Romania zinazalisha kiwango kidogo cha kaboni kutokana na matumizi ya vyanzo vya nishati ya kijani.

Majadiliano yatajikita kwa misingi ya ushahidi wa kisayansi uliokusanywa kwa miaka mingi na kufanyiwa tathimini na wataalam. Hasa kwa kuzingatia ripoti zifuatazo:

- Kumbusho la mwezi Oktoba “uamsho” Ripoti kuhusu ongezeko la joto duniani la kuwa nyuzi joto 1.5˚C, iliyotolewa na IPCC.

2018 Ripoti ya  Pengo la hewa chafuzi, iliyotolewa na UNEP.

2018 Ripoti kuhusu kiwango cha gesi ya viwandani , iliyotolewa na WMO.

2018 Ripoti ya tathimini ya kumomonyoka kwa tabaka Ozoni, iliyotolewa na  WMO na UNEP.

 

7. Unawezaje kufuatilia majadiliano ya COP24?

Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.

Kuna njia nyingi ambazo zinaweza kutuweka sanjari na mjadala huo:

Angalia ukurasa wetu maalum kila wakati kwani tutakukusanyia taarifa zote muhimu kutoka Katowice.

Fuatilia hashtag #ClimateAction kwenye Twitter;

 

 

8. Unawezaje kushiriki na kutoa mchango wako kuhusu mabadiliko ya tabia nchi?

Unaweza kujiunga na Climate Action ActNow.bot ambayo itapendekeza hatua za kuchukuliwa kila siku ili kuiokoa sayari dunia na kujumlisha hatua zitakazochukuliwa kupima matokeo ya kuchukuliwa kwa hatua za pamoja.

Kukushirikisha wengine juhudi unazochukua kuhusu hatua za mabadiliko ya tabianchi kwenye mitandao ya kijamii unaweza kusaidia kuchagiza watu wengi zaidi kuchukua hatua pia.

Zaidi ya hapo mradi wa kiti chako,  uliozinduliwa na makao makuu ya UNFCCC unahakikisha kwamba unaweza kuchangia moja kwa moja kwenye majadiliano ya COP 24. Hivyo hakikisha #TakeYourSeat na kupaza sauti!

 

9. Ipi mifano ya miradi ya Umoja wa Mataifa katika kukabili mabadiliko ya tabia nchi?

 

Watoto katika eneo la Merea Chad wakipanda miti ya Acacia

Kwa sababu Umoja wa Mataifa unahakikisha unachagiza ulinzi endelevu wa mazingira katika mfumo mzima wa kazi zake Idhaa ya Umoja wa Mataifa imekuwa ikiainisha baadhi ya mifano ya miradi inayoungwa mkono na UNEP na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP ambayo inaonyesha njia ya hatua za mabadiliko ya tabianchi: huko Vijijini Ulaya Mashariki, wakulima na wajasiriliamali wanaweza kupunguza kiwango cha hewa chafuzi hatua kwa hatua , huko katika Ukanda wa bonde la ziwa Chad,maelfu ya miti inayohimili ukame inapandwa , nchini Guatemala, kufufua tena uzalishaji wa wakulima wadogowadogo wa kilimo cha kakao nchini Guatemala kunasaidia kushughulikia matatizo na changamoto za kiuchumi na kimazingira, inchini  Bhutan, uwezo wa elimu ya asili umekuwa ukitumika kusaidia maisha na kulinda mazingira, nchini Timor-Leste, kizazi kipya cha miundombinu inayojali mazingira kimaundwa, nako nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC, mabadiliko madogo ya tabia yanaleta mafanikio makubwa.

 

 

10. Kwa nini Umoja wa Mataifa unapanga mkutano mwingine wa mabadiliko ya tabia nchi 2019?

 

Antonio Guterres akiwa New Delhi India katika sherehe za kinara wa mazingira wa UN

Ili kuendeleza kazi ya matokeo ya mkutano wa COP 24, na kuimarisha hatua za mabadiliko ya tabianchi na matarajio katika kiwango cha juu kitakachowezekana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anaitisha mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi Septemba mwaka ujao ikiwa ni mapema kuelekea ukomo wa 2020 kwa nchi kukamilisha mipango yao ya kitaifa ya mabadiliko ya tabianchi. Mkutano huo unalenga kujikita katika miradi ya vitendo kudhibiti uchafuzi wa hewa na kujenga mnepo.

Mkutano huo utaangazia maeneo sita katika kusukuma hatua: mabadiliko ya kuelekea katika nishati mbadala, ufadhili wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na gharama za uchafuzi wa hewa ukaa;  kupunguza gesi ya viwandani; kutumia maliasili kama suluhuu, kuwa na hatua mashinani na miji endelevu; na mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.