Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fursa ya kipekee kwa kila mtu duniani kushiriki katika kuamua mstakabali wa Ulimwengu.

Vijana waliohudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Bonn Ujerumani wakiwa wamebeba kitambaa kilichoandikwa iokoe dunia. Mkutano huo ulihusu mabadiliko ya tabia nchini.
Photo/UNFCCC
Vijana waliohudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Bonn Ujerumani wakiwa wamebeba kitambaa kilichoandikwa iokoe dunia. Mkutano huo ulihusu mabadiliko ya tabia nchini.

Fursa ya kipekee kwa kila mtu duniani kushiriki katika kuamua mstakabali wa Ulimwengu.

Tabianchi na mazingira

Umoja wa mataifa, umetoa taarifa ya kuwataka watu wote kote duniani kwa mara ya kwanza kushiriki moja kwa moja katika mkutano muhimu wa kusaka mustakabali wa dunia kwa kutafuta namna ya kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi.

Taarifa iliyotolewa na sekretarieti ya mkataba wa kimataifa wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC imesema kuwa kuanzia tarehe 2 ya mwezi ujao wa disemba, serikali za mataifa mbalimbali zitakutana nchini Poland kujadili jambo muhimu kwa maisha ya sasa na ya baadaye ya binadamu, mabadiliko ya tabia nchi.

Imesema kuwa maamuzi yatakayochukuliwa, yatagusa kila kiumbe katika dunia hii. Na kwa mara ya kwanza, kila mtu duniani, amealikwa kushiriki katika maamuzi haya. “Umoja wa Mataifa unaanzisha kiti, ‘kiti cha watu’. Kiti hiki kitaweka kwenye moja ya kumbi za Makao makuu ya Umoja wa Mataifa kikiwa na maandishi ‘Take your seat’, yaani ukialikwa kukikalia kiti hiki lakini kwa maana ya kutoa mawazo yako kutokea kokote uliko duniani kuwaelekeza viongozi ni hatua gani za kuchukua ili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.,” imefafanua taarifa hiyo.

Mawazo hayo yatatolewa kwa njia ya mitandao ya kijamii ambapo mtu yeyote popote alipo ataandika ujumbe wake kwa kitambulisha mada #Takeyourseat na kisha mawazo hayo yatakusanywa na kuwasilishwa katika mkutano wa viongozi utakaofanyika nchini Poland.

Mwanamazingira mashuhuri duniani Sir David Attenborough ambaye atawasilisha mawazo ya kiti cha watu anasema hii ni fursa muhimu kwa kila nyanja katika jamii kwa kuwa, “huu utakuwa wakati muafaka wa mamilioni ya watu kote duniani kutuma ujumbe ambao viongozi hawawezi kuupuuza.Wote tunafahamu kuwa mabadiliko ya tabia nchi ni tatizo la dunia na kwa hivyo linahitaji suluhisho la kidunia”

Mwanamazingira huyo amesisitiza kuwa bila kujali utaifa wa mtu, hali aliyonayo, ashiriki katika mjadala huu muhimu wa karne hii.

“Ninamhamasisha kila mtu kukalia kiti hiki na kuchangia sauti yake ili nitakapowasilisha kilichosemwa kiwe kinawakilisha mchanganyiko wa sauti za watu wote duniani,”amesema.

Kuhusiana na tukio hili, Katibu Mtendaji wa UNFCC Patricia Espinosa amesema, “tumeshaona athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi duniani kote kwa ongezeko la joto la digrii moja. COP24 anahitaji kuleta jibu thabiti kwa kufuata haraka ambacho serikali zimekubaliana kukifanya  ili makubaliano ya Paris yaweze kufikiwa”

‘Kiti cha watu’ kinakuja muda mfupi baada ya jopo la Umoja wa Mataifa la mabadiliko ya tabia nchi kutahadharisha kupitia ripoti yake ya ongezeko la joto la nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi, na tahadhari ikienda mbali zaidi na kuonesha kuwa dunia inaelekea katika joto la zaidi ya nyuzi joto 3 licha ya kuwepo wa mkataba wa mkataba wa Paris wa mwaka 2015.