Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua ya China na Ufaransa kuelekea COP24 ni ya kipekee- Guterres

Picha ya pamoja ya viongozi wanaoshiriki mkutano wa G20 huko Buenos Aires nchini Argentina. Picha hiyo imepigwa leo Novemba 30, 2018
UN News/Natalia Montagna
Picha ya pamoja ya viongozi wanaoshiriki mkutano wa G20 huko Buenos Aires nchini Argentina. Picha hiyo imepigwa leo Novemba 30, 2018

Hatua ya China na Ufaransa kuelekea COP24 ni ya kipekee- Guterres

Tabianchi na mazingira

Umoja wa Mataifa umepongeza hatua ya Ufaransa na China ya kuchukua dhima ongozi kuelekea mkutano wa 24 wa mabadiliko ya tabiachi huko Poland, hatua ambayo umoja huo imesema inatia matumaini kwa mamilioni ya watu wanaokumbwa na madhara tabianchi hivi sasa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa pongezi hizo huko Buenos Aires nchini Argentina kandoni mwa mkutano wa mwaka anaohudhuria wa kundi la 20 zinazoongoza kiuchumi duniani, G20.

Amewaeleza waandishi wa habari kwenye mkutano ambao pia wameshiriki Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian na Waziri wa Mambo ya Nje wa China  Wang Yi kwamba dunia sasa inakabiliwa na madhara makubwa kwa maisha ya watu wengi kote ulimwenguni, hususan wale wanaoishi kwenye nchi ambazo ziko hatarini zaidi na iwapo ahadi zaidi hazitaongezwa na kuweka matarajio ya juu hali itakuwa mbaya.

“Katika nchi hizo,  uongozi ambao Ufaransa na China wamechukua kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi bila shak ani muhimu sana na nina furaha mno kuwa nchi mbili hizi zimekutana siku chache kabla ya mkutano wa Katowice ili kusisitiza ushiriki wao na ahadi yao na uongozi wao.”

Katibu Mkuu wa  UN António Guterres akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa G20 huko Buenos Aires Argentina Novemba 29, 2018
UN News/Natalia Montagna
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa G20 huko Buenos Aires Argentina Novemba 29, 2018

Katibu Mkuu amesema mkutano huo wa COP24 unaoanza tarehe 2 mwezi ujao huko Katowice, Poland ni lazima ufanikiwe akiongeza kuwa ni lazima kuweka kichocheo ambacho ni muhimu ili jamii ya kimataifa nayo iongeze kasi kuelekea mwaka 2020 wakati ambapo ahadi zilizotolewa Paris mwaka 2015 zitatathminiwa.

Hivyo Katibu Mkuu amesema… 

“Wakati huo huo  huko Katowice kutakuwepo na fursa ya kuweka ahadi zaidi za kuongeza matamanio yenu ya kile tunataka kufanya kukabili mabadiliko ya tabianchi. Suala kwamba Ufaransa na China leo hii ziko pamoja, kwa mtazamo wangu ni ishara muhimu sana na ni ujumbe muhimu sana kwa jamii ya kimataifa kuwa tunataka kuhakikisha mbio zetu zinashinda kasi ya mabadiliko ya tabianchi, na tutaweza kushinda pambano hili kwa mustakabali wa binadamu na sayari bora.”

GUTERRES AKIZUNGUMZA KWENYE G20

Baadaye Katibu Mkuu ameshiriki katika moja ya mijadala ya G20 ukilenga jinsi ya kuweka mbele maslahi ya watu ambapo amesema hiyo ilikuwa ni kauli mbiu yake wakati akiwa Waziri Mku wa Ureno zaidi ya miongo miwili iliyopita, sambamba na mpinzani wake.

Hata hivyo amesema, katika miongo hiyo ameshuhudia kauli mbiu hiyo ya kuweka mbele maslahi ya watu ikitumika sana na kila wakati. “Tatizo ni kwamba kwa idadi kubwa ya wananchi kwenye jamii zetu hawaoni kama ni kweli maslahi yao yanawekwa mbele badala yake maslahi yao yamepuuzwa.”

Katibu Mkuu amesema suala hilo ni wazi kwani mchanganyiko wa utandawazi na maendeleo ya teknolojia licha ya kuchagiza utajiri na kupunguza umaskini, pia vimeongeza kwa kiwango kikibwa ukosefu wa usawa kwenye jamii.

“ Hali  hii imeleta mkanganyiko kwa jamii na wananchi wanapoteza imani na serikali zao au masharika ya kimataifa kama ninaloongoza,” amesema Katibu Mkuu
 

AKILI BANDIA NI CHANGAMOTO TUJIANDAE

Guterres amesema “tunahitaji kushirikiana ili utandawazi uwe na manufaa kwa wote: Mosi, tunapaswa kuchukua hatua fanisi zaidi ili kupunguza ukosefu wa usawa kwenye jamii zetu kwa sababu mwelekeo huu ni wa kuzidisha pengo la usawa. Hivyo tuweke sera za kifedha, ajira, na zile za hifadhi ya jamii ili kupunguza ukosefu wa usawa.”

Pili amependekeza kujiandaa kwa madhara ya mapinduzi ya nne ya viwanda yanayochochewa na kasi kubwa ya maendeleo ya akili bandia. “Miongo miwili ijayo tutashuhudia pande mbili- ongezeko la fursa za ajira sambamba na kupoteza kwa ajira. Tunahitaji kuwekeza kwenye elimu ya jinsi ya kujifunza mambo mapya.”