Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viashiria vya mabadiliko ya tabianchi na madhara yake vyaendelea 2018

Visiwa vya Tuvalu viko katika hatari ya kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
UNDP Tuvalu/Aurélia Rusek
Visiwa vya Tuvalu viko katika hatari ya kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Viashiria vya mabadiliko ya tabianchi na madhara yake vyaendelea 2018

Tabianchi na mazingira

Hali ya joto duniani imeendelea kuongezeka mwaka 2018 huku wastani wa kiwango cha joto duniani kote ikitarajiwa kushika nafasi ya nne na kuvunja rekodi.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya hali  ya tabianchi duniani iliyotolewa leo na shirika la hali ya hewa duniani, WMO, ikionyesha kuwa miaka 20 yenye joto zaidi ilirekodiwa miaka 22 iliyopita, ambapo iliyoshika viwango vya juu zaidi ni miaka minne iliyopita.

 Ripoti imeweka bayana viashiria vya mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ongezeko la joto kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha bahari, joto na kiwango cha asidi baharini na kuendelea kuyeyuka kwa mabarafu huko ncha ya kaskazini mwa dunia.

Taarifa ndani  ya ripoti hiyo zinatokana na michango kutoka kwa wadau wa Umoja wa Mataifa wakielezea kwa kina madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

 Mathalani ripoti inaonyesha kuwa katika miezi 10 ya mwanzo ya mwaka huu wa 2018, wastani wa kiwango cha joto duniani ulikuwa karibu nyuzi joto 1, kiwango ambacho kilikuwepo kati ya zama za mapinduzi ya viwanda ,(1850-1900).

 “Hatuko kwenye mwelekeo wa kufikia malengo tuliyojiwekea ya kupunguza kiwango cha joto,” amesema Petteri Taalas, Katibu Mkuu wa WMO akiongeza kuwa “mkusanyiko wa hewa chafuzi kwa mara nyingine tena unazidi kuongezeka na kufikia viwango vya juu na iwapo mwelekeo huu utaendelea tunaweza kushuhudia ongezeko la joto hadi kati ya nyuzijoto 3-5 ifikapo  mwishoni mwa karne hii.”

Tuvalu, moja ya visiwa vya Bahari ya Pacific vikiwa kwa wastani chini ya mita mbili juu ya usawa wa bahari. Hali hii imetokana na mabadiliko ya tabia nchi.
UNDP Tuvalu/Aurélia Rusek
Tuvalu, moja ya visiwa vya Bahari ya Pacific vikiwa kwa wastani chini ya mita mbili juu ya usawa wa bahari. Hali hii imetokana na mabadiliko ya tabia nchi.

 

 Katibu Mkuu huyo wa WMO amesema ni vyema kusisitiza tena na tena kuwa “sisi ni kizazi cha kwanza cha kuelewa vyema mabadiliko  ya tabianchi na ni kizazi cha mwisho kuweza kuchukua hatua yoyote dhidi yake.”

Ripoti hii ya WMO ni ushahidi zaidi wa kisayansi ambao unatolewa kuelekea mkutano wa 24 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP24 utakaofanyika mwezi ujao huko Katowice, Poland kuanzia tarehe 2 hadi 14.

Lengo la mkutano huo ni kupitisha miongozo ya utekelezaji wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2015 unaolenga kuhakikisha kuwa ongezeko la kiwango cha joto duniani hakivuki nyuzi joto 1.5.