Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kudhibiti joto katika 1.5°C ni mtaji-IPCC

Picha ya dunia iliyopigwa kwa kutumia sateliti
NASA
Picha ya dunia iliyopigwa kwa kutumia sateliti

Kudhibiti joto katika 1.5°C ni mtaji-IPCC

Tabianchi na mazingira

Tathimini mpya kuhusu mabadiliko ya tabianchi iliyofanywa na jopo la kimataifa la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi IPCC imesema ili kuzuia kupanda kwa joto kwa kiwango cha nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi, kunahitaji mabadiliko ya haraka na yasiyo ya kawaida katika nyanja zote za jamii. Ripoti inasema “Kuzuia joto kuishia nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi, ikilinganishwa na kufikia nyuzi joto 2, siyo tu ni faida kwa wanadamu na mazingira ya asili bali pia kunaweza kuhakikishia jamii endelevu zaidi na ya usawa.

Ripoti hiyo maalumu iliyowekwa wazi leo jumatatu kuhusu kupanda kwa joto kwa nyuzi joto 1.5 imethibitishwa na IPCC mjini Incheon, Jamuhuri ya Korea na itakuwa na mchango muhimu wa kisayansi katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mwezi disemba mjini Katowice, Poland wakati serikali zitakapokuwa zinayapitia tena mkataba wa Paris kuhusu namna ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

"Kutokana na zaidi ya marejeo 6,000 ya kisayansi yaliyoangaziwa na mchango wa kujitolea wa maelfu ya wataalamu na mapitio ya serikali duniani kote, ripoti hii muhimu inathibitisha kwa kina na ufanano na sera ya IPCC," amesema Hoesung Lee, Mwenyekiti wa IPCC.

Waandishi 91 na wahariri kutoka nchi 40 wameiandaa ripoti hii baada ya kupokea mwaliko wa kamati ya mkataba wa kimataifa wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC, ilipoanza kutekeleza makubaliano ya Paris mnamo mwaka 2015.

“Moja ya ujumbe mzito unaopatikana katika ripoti hii ni kuwa tayari tunaona madhara ya kupanda kwa joto kwa nyuzi joto 1 kwa kuona mabadiliko ya hali ya hewa yaliyopitiliza, kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari na kuyeyuka kwa barafu ya Arctic, miongoni mwa mabadiliko,” anasema Panmao Zhai, mwenyekiti mwenza wa kundi la kwanza la IPCC.

Mashine za kufua umeme kwa upepo
UN Photo/Eskinder Debebe)
Mashine za kufua umeme kwa upepo

 

Ripoti pia inaeleza matokeo kadhaa ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaweza kuepukika kwa kuishia kuongezeka kwa joto kutoka nyuzi joto 1.5 ikilinganishwa na 2 au zaidi. Mathalani, kufikia 2100 kupanda kwa kina cha bahari duniani kutashuka kwa sentimita 10 ikilinganishwa na kwenye viwango vya joto vya nyuzijoto 2. Matumbawe yanaweza kupungua kwa asilimia 70 hadi 90 ikiwa kuongezeka kwa joto duniani kutakuwa kwa 1.5 wakati ambapo matumbawe yote zaidi ya asilimia 99 yanaweza kuwa yametoweka yote katika ongezeko la nyuzi joto 2.

"Kupunguza joto kwa nyuzi joto 1.5 kunawezekana ndani ya sheria za kemia na fizikia lakini kufanya hivyo kutahitaji mabadiliko yasiyokuwa ya kawaida," anasema Jim Skea, Mwenyekiti wa kundi la tatu la IPCC III.

“Maamuzi tunayoyafanya leo ni muhimu katika kuhakikisha dunia salama na endelevu kwa kila mmoja, sasa na baadaye. Ripoti hii inawapa watunga sera na watekelezaji, taarifa wanazozihitaji kufanya maamuzi yanayopambana na mabadiliko ya tabia nchi wakati huo huo wakizingatia mazingira husika na mahitaji ya watu. Miaka ijayo huenda ni muhimu zaidi katika historia yetu” anasema Debra Roberts, mwenyekiti mwenza wa kundi la tatu.

Tathimini mpya kuhusu mabadiliko ya tabianchi iliyofanywa na jopo la kimataifa la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi IPCC imesema Matumbawe yanaweza kupungua kwa asilimia 70 hadi 90 ikiwa kuongezeka kwa joto duniani kutakuwa kwa 1.5 wakati a
Kadir van Lohuizen/NOOR/UNEP
Tathimini mpya kuhusu mabadiliko ya tabianchi iliyofanywa na jopo la kimataifa la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi IPCC imesema Matumbawe yanaweza kupungua kwa asilimia 70 hadi 90 ikiwa kuongezeka kwa joto duniani kutakuwa kwa 1.5 wakati ambapo matumbawe zaidi ya asilimia 99 yanaweza kuwa yametoweka yote katika ongezeko la nyuzi joto 2.

IPCC ni nini?

IPCC ni chombo cha Kimataifa ambacho kinahusika na kuchunguza sayansi zinazohusiana na mabadiliko ya tabia nchi. Ilianzishwa na Shirika la mpango wa mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP na Shirika la hali ya hewa duniani WMO mnamo mwaka 1988 ili kuwapatia watunga sera tathmini za kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, madhara yake na hatari gani zinaweza kujitokeza siku za usoni vile vile kuweka mikakati ya kukabiliana na hali baadaye. Ina wanachama 195.

IPCC haifanyi tafiti zake yenyewe bali inapitia maelfu ya tafiti za kisanyansi zinazotolewa kila mwaka na ili kutoa ripoti yake, inawakusanya mamia ya wanasayansi kutoka maeneo mbalimbali ya dunia kujadili na kupitia taarifa zote.