Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia ya nyuklia yaleta mbegu mpya za mpunga na maharage

Mbegu nzuri ya mpunga ni muarobaini wa kutokomeza njaa na umaskini
Nonie Reyes / World Bank
Mbegu nzuri ya mpunga ni muarobaini wa kutokomeza njaa na umaskini

Teknolojia ya nyuklia yaleta mbegu mpya za mpunga na maharage

Tabianchi na mazingira

Aina mpya ya mbegu za mpunga na maharagwe ambazo zinastahimili mabadiliko ya tabianchi zimeanza kusambazwa ili kusaidia wakulima kupanda mazao hayo ambayo ni chakula tegemezi kwenye maeneo hayo.

Shirika la nishati ya atomiki la Umoja wa Mataifa, IAEA, limesema hatua hiyo ilitokana na ukweli kwamba mabadiliko ya tabianchi yanayoaendana na viwango vya joto visivyotabirika, vilisababisha mavuno kupungua na wakulima kutofahamu cha kufanya.

“Mbegu hizo mpya za mpunga pamoja na maharagwe zinahimili kiwango cha juu cha joto katika maeneo yenye ukame,” amesema María Caridad González Cepero, mwanasayansi k utoka taasisi ya kitaifa ya sayansi nchini Cuba, na ambaye alishiriki kwenye utafiti huo unaonufaisha wakulima kutoka nchi lukuki hivi sasa ikiwemo Cuba.

Bi. Cepero amesema mbegu mpya ya mpunga iitwayo ‘Guillemar’, ambayo inastahimili  ukame imeleta manufaa makubwa kwa  wakulima nchini Cuba ambako mavuno yameongezeka kwa asilimia 10.

Taarifa ya IAEA inaesma kuwa mataifa mengine kama India, Pakistan, Ufilipino, Tanzania na Senegal, nayo pia yanajiandaa kuachia mbegu mpya za mpunga zinazoendana na hali ya joto ya nchi zao.

Maharage yakiota kwenye moja ya maeneo ya makao makuu ya FAO, Roma, Italia
FAO/Claudia Nicolai
Maharage yakiota kwenye moja ya maeneo ya makao makuu ya FAO, Roma, Italia

Mradi huo wa utafiti wa miaka mitano wa kusaka mbegu mpya unahusisha wataalamu kutoka IAEA na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO.

Watafiti hao walianza kwa kutafiti ni kwa jinsi gani mpunga na maharagwe vinabadilika na kukua kwa kuzingatia mazingira ya kawaida ya tabianchi na  yasiyo ya kawaida.

Walitumia minururisho kuongeza kasi yay a kawaida ya kuongezeka kwa idadi ya mimea na hatimaye wakachagua ile inayofaa.

Kwa njia hiyo walipata aina lukuki za mazao ya mpunga na maharagwe ambayo yanaweza kuhimili viwango vya joto kupindukia na pia kuwa na mavuno mengi na mojawapo ya mbegu hiyo ni Guillemar inayotumika Cuba.

IAEA  inasema kupata aina mpya za mbegu za mimea kunaweza kusaidia wakulima kupanda mazao mengi ya chakula yanayohimili mabadiliko ya tabianchi, lakini vile vile kusaidia wanasayansi kujifunza zaidi jinsi mimea inaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.