Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kufuatia mashambulio ya anga dhidi ya Syria, UN yatoa kauli

Katibu Mkuu wa UM Antonio Guterres
PICHA/UN/Evan Schneider(maktaba)
Katibu Mkuu wa UM Antonio Guterres

Kufuatia mashambulio ya anga dhidi ya Syria, UN yatoa kauli

Amani na Usalama

Syria! hali ya sintofahamu yaongezeka baada ya mashambulio ya anga kufanyika usiku wa Ijumaa na tayari UN imesema Katiba ya UN lazima izingatiwe na vitendo vya kuleta shari zaidi viepukwe.

Marekani na washirika wake Uingereza na Ufaransa wamefanya mashambulio ya anga nchini Syria.

Kufuatia kitendo hicho, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesihi jamii ya kimataifa ijiepushe na  vitendo ambavyo vitachochea zaidi mgogoro nchini Syria sambamba na machungu kwa raia wa nchi hiyo.

Guterres ametoa wito huo Ijumaa usiku saa chache baada ya Marekani na washirika wake hao kufanya mashambulio ya anga dhidi ya Syria kwenye maeneo yanayohusishwa na silaha za kemikali nchini humo.


Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Guterres amesema “Katiba ya Umoja wa Mataifa imeweka bayana wajibu huo na na Baraza la Usalama lina wajibu wa msingi wa kuendeleza amani na usalama duniani.”


Bwana Guterres ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Usalama kuungana na kutekeleza wajibu huo.


Halikadhalika katika mazingira haya ya sasa amesihi nchi wanachama zijizuie na ziepushe kufanya vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha hali kuwa mbaya zaidi.


Mashambulizi ya pamoja ya anga yaliyofanywa na Marekani na washirika wake yanafuatia shambulio linalodaiwa la kemikali kwenye mji wa Douma nchini Syria wiki iliyopita.


Tayari shirika la kuzuia silaha za kemikali, OPCW limepeleka  ujumbe wake eneo hilo ili kusaka ukweli wa taarifa hizo za matumizi ya silaha za kemikali.


Umoja wa Mataifa ulilaani matumizi ya silaha za kemikali ukisema kuwa ni jambo lisilofaa na iwapo litathibishwa hatua zichukuliwe huku ukitaka Baraza la Usalama liungane katika kukubaliana mfumo wa uwajibishaji wa wahusika wa vitendo vya aina hiyo.