Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ISIL imebadili mbinu na  hiki ni kitisho kipya- Ripoti

Familia ambazo zimekimbia mapigano kati ya ISF na ISIL magharibi mwa Mosul, Iraq
UNICEF/Romenzi
Familia ambazo zimekimbia mapigano kati ya ISF na ISIL magharibi mwa Mosul, Iraq

ISIL imebadili mbinu na  hiki ni kitisho kipya- Ripoti

Amani na Usalama

Ripoti mpya ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu tishio la ugaidi kutoka kikundi cha ISIL imetaja changamoto tatu ambazo zinaendelea kusababisha kundi hilo kuwa tishio la amani na usalama duniani.

Akiwasilisha ripoti hiyo leo mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mkuu wa ofisi ya umoja huo inayohusika vita dhidi ya ugaidi Vladmir Voronkov, ametaja changamoto ya kwanza kuwa ni ISIL kukimbilia mashinani nchini Syria hasa baada ya eneo lao la utawala huko Iraq kusambaratishwa.

“Hivi sasa idadi ya wapiganaji wa ISIL nchini Syria na Iraq inakadiriwa kuwa zaidi ya 20,000 wakiwa wamegawana karibu nusu kwa nusu. Baadhi ya wapiganaji wako uwanja wa vita na wengine wamejificha kwa wananchi wanaosaka huruma na maeneo ya mijini,’ amesema Bwana Vorokonvo akiongeza kuwa ISIL imefanyia ugatuzi masuala yake ya uongozi kwa lengo la kuepuka kupata hasara zaidi.

Bwana Voronkov ametaja changamoto ya pili kuwa ni kurejea na kuwafuatilia wapiganaji wa zamani wa ISIL akisema hivi sasa mwelekeo kwenda Syria na Iraq umepungua lakini changamoto ni stadi ambazo wamezipata wakiwa vitani za kutengeneza mabomu na vilipuzi hatarishi.

Vladmir Voronkov, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia ofisi ya kupambana na ugaidi akihutubia Baraza la Usalama
UN Photo/Manuel Elías
Vladmir Voronkov, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia ofisi ya kupambana na ugaidi akihutubia Baraza la Usalama

Changamoto  nyingine kwa mujibu wa Voronkov ni jinsi mtandao huo wa ISIL unavyobadili muundo wake kutoka ule ulio dhahiri hadi ule wa kificho.

Amesema kuwa “hiki ni kitisho kipya. Mathalani, ni vigumu kufuatilia fedha za ISIL huko Mashariki ya Kati kwa kuwa mifumo ya utawala imekuwa ya kificho. Baada ya mabadiliko ya muundo wake, ISIL bado ina uwezo wa kutuma fedha zake kutoka nchi moja hadi nyingine mara nyingi kwa kupitia nchi za kati hadi kule zinakopaswa kufika.”

Kwa mantiki hiyo amesema ni lazima nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa zipatie nguvu mpya harakati za kukabiliana na tishio hili la ISIL.

Bwana Voronkov amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kwa upande wake amesalia tayari kusaidia nchi wanachama kwenye vita dhidi ya ugaidi ikiwemo ISIL na washirika wake.

Amesema Katibu Mkuu, “anakaribisha hatua ya Baraza la Usalama kuendelea kupatia umuhimu suala hili kwa ushirikiano endelevu na wa kimataifa ndio njia pekee ya kuweza kushughulikia janga la ugaidi.