Silaha za kemikali zadaiwa kutumika tena Syria

8 Aprili 2018

Hadi lini raia  wa Syria wataendelea kuteseka? Mapigano yanashika kasi kila uchao na maazimio ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kusiginwa.

Raia huko Douma, Mashariki mwa Ghouta nchini Syria yadaiwa wameshambuliwa kwa silaha za kemikali katika mashambulio ya saa 36 zilizopita.

Mashambulio hayo yamedaiwa kusababisha vifo vya raia pamoja na kuharibu miundombinu ya kjamii ikiwemo vituo vya afya.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ingawa umoja huo hauna uwezo wa kuthibitisha madai hayo ya matumizi ya silaha za kemikali huko Douma, bado kitendo hicho iwapo kitathibitishwa ni cha kuchukiza na kinatahika uchunguzi wa kina.

Watoto wakiteka maji huko Douma, mji ulioko kwenye eneo la Ghouta Mashariki, nje kidogo ya mji mkuu wa Syria, Damascus.
UNICEF/Bassam Khabieh
Watoto wakiteka maji huko Douma, mji ulioko kwenye eneo la Ghouta Mashariki, nje kidogo ya mji mkuu wa Syria, Damascus.

Halikadhalika amesikitishwa na kuibuka tena kwa mapigano makali ikiwemo mjini Damascus, licha ya azimio namba 2401 la mwaka huu la Baraza la Usalama lililitoka mapigano yakomeshwe mara moja.

Bwana Guterres amerejelea kuwa suluhu ya kijeshi haina nafasi kwenye mzozo wa Syria na kwamba ni vyema raia walindwe.

Katibu Mkuu kupitia taarifa ya msemaji wake amesihi pande kinzani kwenye mzozo huo kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu ikiwemo kutoa fursa kwa misaada ya kibinadamu kufikishwa kwa wahitaji kwa mujibu wa maazimio ya Baraza la Usalama.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter