Skip to main content

Silaha za kemikali zimetumika Douma au la?

Picha: WHO_EPA/Stringer
Mtoto atibiwa baada ya mashambulio ya kemikali nchini Syria (Maktaba).

Silaha za kemikali zimetumika Douma au la?

Amani na Usalama

Uchunguzi umeanza kuweza kubaini iwapo silaha za kemikali zimetumika kwenye shambulio dhidi ya raia huko Douma, nchini Syria.

Shirika la kimataifa la kupinga matumizi ya silaha hizo, OPCW limesema pamoja na kufuatialia kwa karibu tukio hilo la jumamosi, tayari jopo lake liko kwenye mchakato wa kukusanya taarifa kutoka vyanzo vilivyopo kubaini ukweli wa sakata hilo.

Mkuu wa OPCW Ahmet Üzümcü amesema matokeo ya uchunguzi huo yatawasilishwa mbele ya nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa kupinga silaha za kemikali.

Yaripotiwa kuwa shambulio hilo lilifanyika jumamosi kwenye mji huo wa Douma ulioko Ghouta Mashariki, karibu na mji mkuu Damascus, ambapo mji huo wa Douma bado uko chini ya wapinzani wa serikali ya Syria.

Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani kitendo hicho akisema ni kinyume na azimio la Umoja wa Mataifa namba 2401 la mwaka huu wa 2018 linalotaka siyo tu kusitishwa kwa mapigano bali pia kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.