Nimeghadhibishwa na matumizi ya silaha za kemikali Syria

10 Aprili 2018

Nimeghadhibishwa sana na ripoti za kuendelea kwa matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres , huku akirejea kulaani vikali matumizi yoyote ya silaha za kemikali dhidi ya raia.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Guterres amesma, thibitisho lolote la matumizi ya silaha za kemikali na upande wowote kwenye mzozo, katika mazingira ya aina yoyote ni uhalifu na ukiukaji bayana wa sheria za kimataifa.

Ameongeza kuwa madai makubwa ya sasa yanahitaji uchunguzi wa kina, usio egemea upande wowote , ulio huru na wa kitaalamu.

Na kwa mantiki hiyo amesisitiza uungaji wake mkono wa shirika la kimataifa la kupinga matumizi ya silaha za kemikali (OPCW) kuchunguza madai hayo.

Amehimiza kuwa desturi za kupinga matumizi ya silaha za kemikali lazima ziheshimiwe, na ameliomba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kutimiza wajibu wake na kushikamana katika suala hili.

Pia ameliomba baraza hilo kuongeza mara mbili juhudi zake ili kuafikiana mfumo wa uwajibikaji dhidi ya matumizi ya silaha hizo, na kwamba yuko tayari kusaidia juhudi hizo.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter