Skip to main content

Raia wakiteketea, Syria yaendelea kugonga vichwa UN

Kikao cha Baraza la Usalama
UN /Mark Garten
Kikao cha Baraza la Usalama

Raia wakiteketea, Syria yaendelea kugonga vichwa UN

Amani na Usalama

Kwa mara nyingine tena Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kujadili hali ya usalama Mashariki ya Kati, Syria ikichukua nafasi kubwa zaidi ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema hali ya amani ni shaghalabaghala.

Amewaambia wajumbe 15 wa chombo hicho kuwa Syria ni tishio kubwa zaidi la amani na usalama duniani ambapo mapigano yanayoendelea yanahusisha siyo tu pande kinzani ndani ya nchi bali pia majeshi ya mataifa kadhaa bila kusahau wapiganaji mamluki wa kigeni.

Guterres amesema kwa miaka 8 sasa wasyria wako katika sintofahamu kubwa wakishuhudia ukatili na uhalifu wa wa kutisha.

(Sauti ya Antonio Guterres)
 

“Katika nyakati za matumaini, Baraza la Usalama lilipitisha azimio 2401 kutaka pande zote zisitishe uhasama bila kuchelewa ili misaada ya kibinamu ifikie walengwa. Kwa bahati mbaya, Hakuna sitisho la chuki limetokea. Huo ndio mkwamo wa Syria hii leo.”

Bwana Guterres akageukia sakata la madai ya matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria uchunguzi wa kina unahitajika na la msingi ni uwajibishaji wa watakaobainika kuhusika. Kwa mantiki hiyo amesema..

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Kuongezeka kwa mvutano na kutokuwa na uwezo wa kukubaliana juu ya kuanzishwa kwa mfumo wa uwajibishaji wahusika kunaweza kuchagiza zaidi operesheni za kijeshi. Katika mazungumzo yangu nanyi, hususan wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama nimeonyesha hofu yangu kubwa kuhusu hatari ya mkwamo wa sasa na kusisitiza haja ya kuepusha jambo hilo kupanuka na kushindwa kudhibitika. Ni wajibu wetu sote kukomesha hali hii.”

Katika kikao hicho Kuwait ambayo nayo ni mjumbe wa Baraza la Usalama imetaka kura turufu isitumike pindi rasimu ya azimio linalotaka kupitishwa linalenga kuepusha ukiukwaji wa haki wa binadamu.