Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima tuwe na muafaka kuhusu uhamiaji: Lajčák

Rais wa Baraza Kuu Miroslav Lajčák akihutubia mkutano wa baraza kuu kuhusu vipaumbele vyake kwa mwaka 2018. Picha na: UN/Manuel Elias

Lazima tuwe na muafaka kuhusu uhamiaji: Lajčák

Muafaka ni lazima ufikiwe na mataifa yote duniani juu ya mkakati wa kimataifa kuhusu uhamiaji, amesema leo Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Miroslav Lajčák ameyasema hayo kwenye makao makuu ya Umoja hu mjini New York,alipokuwa akiainisha vipaumbele vya baraza kuu kwa mwaka huu akiwa kama rais.

Amesema matokeo muhimu yameshafikiwa, lakini kuna mambo ambayo ni lazima yafanyike kabla ya muhula wake kumalizika mwezi Septemba. Katika suala la kudumisha amani duniani amesema uzuiaji migogoro, kujenga mshikamano, ufadhili zaidi na mchangamano mzuri ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa ni muhimu sana.

Pia amehimiza haja ya kupiga hatua katika utekelezaji wa malengo 17 ya maendeleo endelevu au SDG’s. Lakini kipaumbele chake cha kwanza ni kupata muafaka wa mkakati wa kwanza kabisa wa kimataifa kuhusu uhamiaji ambao unajadiliwa na serikali zote ili kupunguza madhila kwa watu takribani milioni 65 duniani waliolazimika kukimbia makwao.

Ameongeza kuwa majadiliano ya mwisho kuhusu muafaka huo yatafanyika Julai na yanaaza Februari 20.

(SAUTI YA MIROSLAV LAJCAK) 

"Kutakuwa na mtihani kwetu sote..wote itabidi tufikie muafa. Sote itabidi kuchagiza msaada nyumbani. Wote itabidi kujivuta ili tukutane kati.Kwa sababu ni lazima tuwe na muafaka ifikapo Julai. Hii ni ahadi tuliyojiwekea sisi wenyewe na kwa watu kote duniani. Hatuwezi kutoitimiza.”