Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuna imani na operesheni za ulinzi wa amani za UM:Trudeau

Mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa nchi wachangiaji wa vikosi kwenye Umoja wa Mataifa ukikunja jamvi Vancouver Canada. Picha na UM/Matthiew wells

Tuna imani na operesheni za ulinzi wa amani za UM:Trudeau

Ulinzi wa amani una uwezo wa kuibadili dunia lakini ubunifu wa hali ya juu unahitajika ili kuzifanya operesheni za Umoja wa Mataifa kuwa na ufanisi katika miaka ijayo.

Hayo ni kwa mujibu wa waziri mkuu wa Canada , Justin Trudeau,katika hotuba yake kwenye mkutano wa umoja wa Mataifa wa mawaziri wa ulinzi unaokuja jamvi leo mjini Vancouver.

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa kwenye mkutano huo amewaambia mawaziri hao kutoka nchi takribani 80 zinazoshiriki operesheni za ulinzi za Umoja wa Mataifa kwamba changamoto zinazokabili operesheni hizo zinaweza kutatuliwa lakini sio na Umoja wa Mataifa pekee.

Jean-Pierre Lacroix, amesema changamoto kwa sasa ni kubwa kuliko wakati mwingine wowote

(LACROIX CUT)

“Tunaweza kuzikabili changamoto hizi , hatuwezi kufanya hivyo peke yetu , tunawahitaji, tunahitaji msaada wenu, tunahitaji msaada wa nchi wachangiaji wa vikosi, tunahitaji msaada wa asasi za kiraia na viongozi shupavu ambao wanaweza kutusaidia katika ulinzi na kusaidia Umoja wa Mataifa. Hivyo sisi kwenye Umoja wa Mataifa tutafanya kazi bila kuchoka kuhakikisha operesheni za ulinzi wa Amani zinakuwa thabiti na zenye ufanisi.”

Ameongeza kuwa mtazao unahitajika katika masuala ya vipaumbele kama kusaka suluhu ya kisiasa katika migogoro sugu, na kuongeza ushiriki wa wanawake ili walinda amani wawe chachu kweli ya amani na haki.

image
Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau akihutubia mkutano wa mawaziri wa ulinzi mjini Vancouver Canada. Picha na UN News/Matthiew wells.
Naye waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau ametoa ahadi yenye lengo la kuziba mapengo katika operesheni za hatari kwenye nchi kama Mali na Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo DRC.

Pia amezindua kanuni mpya za Vancouver za kuzuia askari watoto hata kufikia katika uwanja wa vita, na ameahidi kwamba Canada itafanya kila iwezalo kusaidia kubadilisha operesheni za kulinda Amani za Umoja wa Mataifa.

(TRUDEAU CUT)

“Operesheni za amani za kisasa huja na baadhi ya changamoto kubwa, maamuzi magumu na athari kubwa ya tunachofanya. Lakini kujitolea kwetu kwa jitihada kunasaidia, kwa sababu tunaamini katika ulinzi wa amani. Tumeona uwezo wake wa kubadilisha na tunajua hakuna zawadi kubwa zaidi ambayo tunaweza kuwaacha watoto wetu na wajukuu wetu kuliko amani ya kweli na ya kudumu. Hivyo hebu tuwe na ujasiri, na hebu tuwe wabunifu. Hebu tujaribu mambo mapya. Hebu tuwe mabadiliko tunayohitaji, kujenga ulimwengu wa amani pamoja. "

Pia ameahidi kuongeza ushiriki wa wanawake kama njia muafaka ya kukabili mizizi ya migogoro, mafunzo na uwezo wa safari za anga kwenye kituo cha Umoja wa Mataifa Afrika Mashariki.