Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uharibifu unaochangiwa na migogoro unaathiri elimu Afrika:UNICEF

Mtoto anasoma kitabu karibu na Mlango wa shule ya muda nchini Sudan Kusini. Picha: UNICEF

Uharibifu unaochangiwa na migogoro unaathiri elimu Afrika:UNICEF

Shule zisizo salama au zilizoharibiwa, kutokuwepo kwa waalimu na safari za hatari kuelekea shuleni ni miongoni mwa uharibifu unaochangiwa na migogo ambao unaathiri mustakbali wa elimu kwa vijana barani Afrika, kwa mujibu wa utafiti mpya wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Matokeo ya utafiti huo uliofanyika katika nchi nne, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Uganda, Chad na Nigeria kwa kuhusisha kura iliyopigwa na vijana 128,000 yamewasilishwa leo kwenye tukio la mazungumzo maalumu yanayofanyika mjini Brussels Ubelgiji kabla ya mkutano baina ya Muungano wa Afrika AU na Muungano wa Ulaya EU.

Tukio hilo limeandaliwa na UNICEF na ofisi ya mkurugenzi mkuu wa tume ya Muungano wa Ulaya kwa ajili ya ulinzi wa raia na operesheni za misaada ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa UNICEF athari kwa elimu zinazosababishwa na migogoro zimeongezeka kwa asilimia 76 nchini Nigeria na hadi asilimia 89 katika baadhi ya maeneo ya Kaskazini mwa Uganda.

Na karibu asilimia 50 ya waliohusishwa kwenye utafiti huo wamesema sababu nyingine kubwa ni shule kulazimika kufungwa au zilizoharibiwa na machafuko zinawafanya wengi kutopata elimu.