Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 335 zachangishwa kusaidia warohingya huko Bangladesh

Dola milioni 335 zachangishwa kusaidia warohingya huko Bangladesh

Harakati za kusaidia janga linalokumba waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar zimepatiwa usaidizi hii leo kufuatia mchango wa dola milioni 335 kutoka kwa wahisani.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi ametaja kiasi hicho cha fedha huko Geneva, Uswisi hii leo mwishoni mwa mkutano wa kuchangisha fedha za kusaidia wakimbizi hao waliokimbilia Bangladesh.

Amesema idadi hiyo ya fedha ni mchango wa kuanzia tarehe 25 mwezi Agosti mwaka huu hadi leo ahadi na fedha zilizotangazwa leo kwenye kikao hicho na zinatoka nchi wanachama 35 wa Umoja wa Mataifa, mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF na mashirika mengine.

(Sauti ya Grandi)

“Walioahidi, watimize ahadi hizo mapema iwezekenavyo, na tuhamasishe wale walioahidi kutoa ahadi au watahamasisha ahadi katika siku chache zijazo wafanye hivyo kadri inavyowezekana. Tunashukuru kila mtu.”

Wakati huu ambapo warohingya waliokimbilia Bangladesh kutokana na mateso, ubakaji na mauaji ikifikia zaidi ya 550,000, Bwana Grandi ameomba mshikamano wa leo uendelee akisema..

(Sauti ya Grandi)

“Natumai kuwa warohingya ambao kwa muda mrefu wamekuwa wapweke, leo wataona si wapweke sana kwa kuwa mshikamano huu wa kimataifa uko nao. Nasihi mshikamano  huu usiwe wa muda mfupi. Mshikamano huu utahitajika kwa muda iwapo tunataka kupatia suluhu tatizo la muda mrefu la ukimbizi  na ukosefu wa utaifa katika zama za zetu za sasa.”

Mkutano huo uliandaliwa kwa pamoja na Muungano wa Ulaya na Kuwait kwa kushirikiana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu maafa, OCHA, shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM na lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.