Machafuko yasiokwisha Yemen yatishia elimu kwa watoto million 4.5

18 Oktoba 2017

Zaidi ya miaka miwili na nusu ya machafuko nchini Yemen kwa mara nyingine yameiweka elimu ya watoto milioni 4.5 njia panda, na hivyo kuongeza orodha ya madhila yanayowakabili watoto.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF , robo tatu ya waalimu hawajalipwa mishahara yao kwa karibu mwaka sasa na machafuko yamesababisha shule moja kati ya 10 nchini nzima kufungwa.

Shirika hilo limeongeza kwamba hadi kufikia Julai mwaka huu shule 1600 ama zimeharibiwa kwa kiasi fulani au kusambaratishwa kabisa na zingine 170 zinatumiwa kwa masuala ya kijeshi au malazi kwa familia zilizotawanywa na mchafuko.

Inakadiriwa kwamba watoto milioni mbili nchini humo hawako shuleni na kwa watoto ambao wanahudhuria shule utapia mlo, jinamizi la kutawanywa na ghasia zinazoendelea vimeathiri uwezo wao wa kujifunza.

Wakati huu UNICEF na washirika wakijitahidi kuhakikisha watoto wanapata elimu nchini humo imetoa wito kwa wahisani kusaidia kuwalipa waalimu, wahudumu wa afya na wafanyakazi wengine wa umma wanaotoa huduma muhimu kwa watoto.