Hakuna mtoto anayezaliwa akiwa gaidi, vichocheo vitatuliwe - Mohammed

21 Septemba 2017

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amesema kwa kipindi cha miaka minane dunia imeshuhudia madhila ya watu wa Cameroon, Chad, Niger na Nigeria katika mikono ya kundi la Boko Haram ambapo ghasia kutokana na kundi hilo zimewaacha watu milioni kumi katika ukanda wa Ziwa Chad wakihitaji msaada wa kibinadamu.

Bi. Mohammed akizungumza katika mkutano wa mawaziri kuhusu Nigeria na Ziwa Chad ulioandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, amesema madhila ya watu wa ukanda huo ni msumari wa moto juu ya kidonda kwani walikuwa wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo umasikini, ukosefu wa huduma muhimu na mabadiliko ya tabianchi mbali ya mateso kutoka kwa kundi hilo la kigaidi.

Kufikia sasa watu milioni 2.3 wamefurushwa makwao nao milioni tano wana mahitaji ya chakula na bidhaa za msingi huku watoto nusu milioni wakikabiliwa na utapiamlo uliokithiri na hivyo kuwa katika hatari ya kupoteza kizazi kizima.

Naibu Katibu Mkuu huyo ametambua juhudi za mashirika ya kibinadamu na jumuiya ya kimataifa hata hivyo amesema juhudi zaidi zinahitajika…

“Mimi binafsi nilikulia Maiduguri, ambako kundi la Boko Harama limeshamiri na najua wazi kwamba hamna mtoto anayezaliwa akiwa mgaidi. Watoto na vijana  wanachukuliwa na kushawishiwa kuchukua misimamomikali na mazingira yao yanachangia wao kuwa katika hali walioko sasa, wanapoteza maisha yao na mustkabali wao. Ni lazima serikali zichukue hatua kukabiliana na mizizi inayosababisha ukatili huo ikiwemo masuala ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kidini.”