Katika kulinda raia tuzibe ufa badala ya kujenga ukuta- Guterres

6 Septemba 2017

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekutana kujadili ulinzi wa raia ambapo Katibu Mkuu António Guterres amewasilisha ripoti yake ya kwanza kuhusu mada hiyo.

Akihutubia kikao hicho mjini New York, Marekani,  Bwana Guterres amesema ripoti hii inakuja wakati kunahitajika juhudi za pamoja kwa ajili ya kuzuia mauaji ya halaiki, ukatili wa kivita, mauaji yanayolenga kundi moja na ukatili dhidi ya utu na kuongeza kwamba..

“Uhalifu huo haupungui, raia wakiwemo wanawake na watoto wanalengwa au ni wahanga wa mashambulizi ya kiholela, na matokeo yake ni idadi kubwa ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani. Kuwajali ilikuwa wajibu wangu katika wadhifa wangu wa awali. Sasa kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nina wajibu wa kushughulikia sababu za wao kukimbia: mizozo na uhalifu.”

Guterres ametoa mapendekezo ya kubadili taswira iliyopo sasa akisema kwamba Umoja wa Mataifa unapaswa kujikita katika kuzuia badala ya kusubiri hali kuwa mbaya pia kuweka ajenda yenye hatua za vitendo.

Aidha amegusia jukumu la Baraza la Usalama akisema…

“Hebu tujadili wazi kuhusu wajibu wa Baraza la Usalama katika kuzuia uhalifu. Kwa kukabiliana na kutoelewana na upungufu wa awali na kuimarisha juhudi zetu na kuibuka kutoka kwenye tofauti za kisiasa na kutoaminiana ambako mara kwa mara ni mwanzo wa udhaifu wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia majanga.”

 Kwa mantiki hiyo amependekeza muongozo wa maafikiano ya kongamano la kimataifa kwa kila taifa kulinda raia wake na nchi zingine kuingilia kati pale nchi husika inashindwa kuzuia uhalifu.

Aidha ametaka Umoja wa Mataifa uchukue hatua ya pamoja kwa mujibu wa katiba yake wakati huu ambapo kunashuhudiwa ukatili katika maeneo mengi ya dunia.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter