Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takribani asilimia 50 ya wanawake Tunisia waonja ukatili

Takribani asilimia 50 ya wanawake Tunisia waonja ukatili

Tunisia imepiga hatua kubwa kwa kupitisha kwa mara ya kwanza sheria ya kitaifa ya kupambana na ukatili dhidi ya wanawake tarehe 26 July mwaka huu, ukatili unaoathiri asilimia 50 ya wanawake nchini humo, limesema leo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UNWomen . Taarifa kamili na Amina Hassan..

(Selina Amina)

Sheria hiyo iliyochukua muda kupitishwa, imekubaliwa kwa kura 146 kati 217 na bila ya kupingwa, na ina mbinu mseto za kuzuia ukatili na kutoa msaada kwa waathirika.

UNWomen ambayo pia imeshiriki katika mapitio ya sheria hiyo kabla ya kupitishwa, imesema mbali na unyanyasaji wa kimwili, sheria hiyo itakabiliana na aina zote za unyanyasaji dhidi ya wanawake ikiwemo wa kiuchumi, kijinsia, kisiasa na kisaikolojia. Vile vile sheria hiyo inatoa utaratibu mpya wa ulinzi ambao utawezesha waathirika kupata huduma muhimu na msaada wa kisheria na kisaikolojia.

Sheria hiyo pia imeondoa ukwepaji sheria kwa wahalifu, kwa kurekebisha kifungu namba 227 cha kanuni ya adhabu, ambacho kinamsamehe mhalfiu wa ukatili wa kingoni iwapo atakubali kumuoa muathirika.

Imesema wakati kupitisha sheria kunaashiria hatua muhimu na mwelekeo sahihi, utekelezwaji wake utakuwa muhimu zaidi katika kubadili maisha ya wanawake.