Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzani uko juu katika mapambano dhidi ya VVU japo watu muhimu bado wako hatarini

Mzani uko juu katika mapambano dhidi ya VVU japo watu muhimu bado wako hatarini

Hatua kubwa imefikiwa katika vita dhidi ya virusi vya HIV kwa mujibu wa wataalamu wa afya wa Umoja wa Mataifa ambao wanasema zaidi ya nusu ya watu wote wanaougua ukimwi sasa wana fursa ya matibabu.

Tangazo lililotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya ukimwi UNAIDS lina takwimu mpya zinazoonyesha kwamba takribani watu milioni 37 wanaishi na virusi vya HIV hadi kufikia mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la asilimi 11 tangu mwaka 2010.

Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika zimekuwa msitari wa mbele katika kupunguza maambukizi kwa karibu asilimia 40 katika baadhi vya visa, lakini watoto na jamii zisizojiweza wanasalia katika hatari kama anavyofafanua Dr Peter Ghys kutoka UNAIDS

(SAUTI YA DR PETER)

Tunashuhudia matibabu kwa watoto yako nyuma ukilinganisha na matibabu ya watu wazima na bila shaka matibabu miongoni mwa watoto yana changamoto kwa sababu kwa upande mmoja watoto wanapimwa mara tu baada ya kuzaliwa au wiki chache baada ya kuzaliwa hivyo ni rahisi kubaini watoto walioathirika na kuwapa matibabu lakini ni changamoto kwa wale ambao wamepita kidogo umri wa utoto.