Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto 1 kati ya 10 hakupata chanjo 2016 duniani

Mtoto 1 kati ya 10 hakupata chanjo 2016 duniani

Kote ulimwenguni watoto milioni 12.9, sawa na mtoto mmoja kati ya kumi hawakuchanjwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la afya ulimwenguni WHO na lile la kuhudumia watoto UNICEF.Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Kwa mujibu wa mashirika hayo hii inamaanisha kwamba watoto hao walikosa dozi ya kwanza ya chanjo ya pepopunda (DTP) na hivyo kuwaweka katika hatari ya ugonjwa huo unaosababisha vifo.

Aidha takriban watoto milioni 6.6 waliopata dozi ya kwanza ya DTP hawakumaliza dozi tatu zinazohitajika za chanjo hiyo mwaka 2016.

Ripoti pia inaonyesha kwamba chanjo huzuia vifo kati ya milioni 2-3 kila mwaka dhidi ya magonjwa kama vile: mkamba, pepopunda, kifaduro na surua.

Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo, watoto wengi wanaokosa chanjo wanakosa huduma zingine muhimu za afya.

Nchi nane ikiwemo: Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Equatorial Guinea, Nigeria, Somalia, Sudan Kusini, Syria na Ukraine zilitoa chanjo kwa watoto chini ya asilimia 50 mwaka 2016.