Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu mpya yaepusha janga la kibinadamu Sudan Kusini

Mbinu mpya yaepusha janga la kibinadamu Sudan Kusini

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS umesema mbinu mpya ya ulinzi wa amani imesaidia kuzuia janga la kibinadamu kwenye jimbo la Upper Nile nchini humo.

Mbinu hiyo inahusisha ushirikiano kati ya walinda amani na wafanyakazi wa misaada ambapo UNMISS imesema imetumika kwenye kijiji Aburoc ambako mzozo ulisababisha watu 70,000 kukimbia makazi yao.

Mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini David Shearer ambaye pia ni mkuu wa UNMISS amesema wakimbizi hao walikuwa na mahitaji ya kibinadamu ambapo mbinu hiyo ilisaidia.

Amesema walinda amani 80 kutoka Rwanda walipelekwa haraka eneo hilo ili kuwezesha wahudumu wa misaada kusambaza misaada bila hofu ya ukosefu wa usalama.

(Sauti ya David Shearer)

“Ni jambo ambalo hatujawahi kufanya. Ni jambo ambalo walinda amani wetu hawajulikani kwa kulifanya.. kupanda helikopta, kuruka angani ndani ya muda mfupi na kuweka kituo kwenye eneo linaloweza kuwa na hatari na kuendelea na kazi ya kuwezesha wengine kufanya kazi za misaada.”

Bwana Shearer amesema ni matumaini yake kuwa mbinu hiyo itaigwa na operesheni nyingine za ulinzi wa amani.