Ukatili dhidi ya wazee waongezeka limeonya shirika la WHO

15 Juni 2017

Shirika la afya ulimwenguni WHO limeonya kwamba ukatili dhidi ya wazee unaongezeka kote duniani. Katika kuadhimisha siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee duniani, utafiti mpya uliofadhiliwa na WHO na kuchapishwa na jarida la kimataifa la afya la Uingereza, Lancet umebaini kwamba mzee 1 kati ya 6 anakabiliwa na ukatili.

Takwimu hizo ni kubwa kuliko zilivyotarajiwa hapo awali na zinatazamiwa kuongezeka limesema shirika hilo. Watu wenye umri wa miaka 60 au zaidi mara nyingi hukabiliwa na unyanyasaji wa kisaikolojia, kifedha, kimwili na baadhi ya visa vya unyanyasaji wa kingono.

Takwimu hizo zimetokana na tafiti 52 zilizofanywa katika nchi 28, kwenye maeneo tofauti ikiwemo mataifa 12 ya kipato cha chini na cha wastani. WHO inasema juhudi zaidi zinahitajika kuzuia na kukabiliana na ongezeko la aina tofauti za ukatili dhidi ya wazee.

Inatarajiwa kwamba ifikapo mwaka 2050 idadi ya watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi itaongezeka mara mbili na kufikia bilioni 2 kote duniani na wengi wao watakuwa wakiishi kwenye nchi za kipato cha chini na cha wastani.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter