Ban awa na mazungumzo na Rais Yudhoyono wa Indonesia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ambaye yuko ziarani barani Asia, amekuwa na mazungumzo na Rais Susilo Bambang Yudhoyono wa Indonesia na kumshukuru kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa sita wa kimataifa wa ustaarabu duniani.
Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema pamoja na shukrani hizo wawili hao wamejadili masuala kadhaa ikiwemo ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015 ambapo Rais Yudhoyono ni mwenyekiti mwenza wa jopo hilo.
Ban ameshukuru Yudhoyono kwa uongozi wake kwenye jopo hilo akishukuru pia Indonesia kwa mchango wake katika utekelezaji wa vipaumbele vya Umoja wa Mataifa na ushiriki wake kwenye ulinzi wa amani.
Halikadhalika wamejadili uchaguzi wa hivi karibuni Indonesia, hali ya Mashariki ya Kati, Myanmar, Ukraine na Iraq pamoja na ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muugano wa nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN.
Taarifa hiyo pia imethibitisha ushiriki wa Rais Yudhoyono kwenye mkutanowa viongozi kuhusu mabadiliko ya tabianchi ambao umeandaliwa na Katibu Mkuu Ban na utafanyika New York tarehe 23 mwezi ujao.