Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Japan yatoa dola milioni 3.5 kusaidia lishe Nigeria

Japan yatoa dola milioni 3.5 kusaidia lishe Nigeria

Shirika la Mpango wa Chakula, WFP leo limekaribisha mchango wa dola milioni 3.5 za kimarekani kutoka Japan kusaidia watu 160,000 waliosambaratishwa na mapigano ya Boko Haram Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Mchango huo utawezesha WFP kupeleka chakula haraka katika majimbo ya Borno na Yobe ambako mapigano hayo yamesababisha ukosefu mkubwa wa chakula na hatari ya njaa katika maeneo mengine.

WFP imesema hivi sasa takriban watu milioni 4.7 wanahaja kubwa ya chakula katika majimbo ya Borno, Yobe na Adamawa, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 5.1 ifikapo mwezi Juni.

Katika miezi minne, tayari WFP imeweza kuwafikia watu milioni moja walio katika mazingira magumu hususan wanawake na watoto, na inatarajia kuongeza idadi hiyo hadi milioni 1.8 kwa mwezi.