Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 27 katika nchi nne za Afrika hawana maji safi na salama- UNICEF

Watu milioni 27 katika nchi nne za Afrika hawana maji safi na salama- UNICEF

Uhaba wa maji, ukosefu wa huduma za kujisafi na tabia zisizo sahihi za kujisafi zinaongeza tishio kwa watoto ambao tayari wanakabiliwa na unyafuzi huko kaskazini-mashariki mwa Nigeria, Somalia, Sudan Kusini na Yemen.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema hayo hii leo likiongeza kuwa takribani watu milioni 27 katika nchi hizo nne zilizo katika tishio la njaa kali wanatumia maji yasiyo safi na salama, jambo linaloweza kusababisha wapate kipindupindu, watoto wakiwa hatarini zaidi.

Mkurugenzi wa miradi ya dharura UNICEF Manuel Fontaine amesema miundombinu ya maji safi kwenye nchi hizo imeharibiwa akitolea mfano Sudan Kusini ambako nusu ya vyanzo vya maji safi na salama havifanyi kazi ilhali Somalia vyanzo vya maji vimekauka.

Kwa mantiki hiyo UNICEF na wadau wamechukua hatua kusambaza maji kwenye maeneo yenye mahitaji na kuendesha kampeni za kujisafi akisema huko Somalia wanalenga watu milioni 1.5 ambapo kila mmoja anapatiwa lita saba na nusu za maji kila siku kwa siku 90 hadi mvua zianze kunyesha mwezi ujao.

UNICEF imesema kuwa hata kama mtoto mwenye utapiamlo atapatiwa lishe bora, bado haitasaidia iwapo maji anayokunywa si safi na salama.