Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu , msaada na upendo ni muhimu kwa wenye down syndrome:

Elimu , msaada na upendo ni muhimu kwa wenye down syndrome:

Leo ni siku ya kimataifa ya ugonjwa unaoathiri uwezo wa kujifunza au down syndrome. Kauli mbiu mwaka huu ni “sauti yangu, jamii yangu” lengo likiwa kuwawezesha watu wenye ugonjwa huo kupaza sauti zao, kusikilizwa na kushawishi sera za serikali na hatua za kujumuishwa katika jamii.

Akizungumza katika mjadala maalumu wa kuadhimisha siku hii kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York , mkurugenzi wa jumuiya ya kimataifa ya ugonjwa unaoathiri uwezo wa kujifunza Andrew Boys, amesema kila siku sauti za watu wanaofanya kazi, kuishi na kuwasaidia wagonjwa wa down syndrome inazidi kupazwa, hasa katika juhudi za kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa huo, ina maanisha nini kuwa nao na jinsi gani watu wenye ugonjwa huo wanajukumu muhimu katika maisha yetu na jamii.

Ameongeza kuwa mjadala wa leo ni muhimu sana kwa sababu

(SAUTI YA BOYS CUT)

“Unawasikiliza watu wenye down syndrome, wachagizaji, wazoefu na wataalamu wakijadili kwa nini ni muhimu watu wenye ugonjwa unaoathiri uwezo wa kujifunza na wasaidizi wao kuzungumza na kuwachagiza watunga sera wa kikanda, kitaifa na kimataifa , na kuelezea sera gani muhimu zinazoathiri maisha ya watu wenye ugonjwa huo, na kuwahakikishia ujumuishwaji kamilifu katika jamii kama sera hizo zitatekelezwa.”

Naye Amany Abu Middain kutoka Gaza, mwanamke wa kwanza kupata kibali cha kuendesha ndege za abiria Gaza, mama mwenye mtoto aliye na down syndrome na mwanaharakati wa kupigania haki za watoto wenye ugonjwa huo kupitia shirika lisilo la kiserikali la “Right to live society lililoko Gaza Palestina, akichangia mjadala huo ametaja mambo ya muhimu yanayohitajika kwa watu wenye ogonjwa huo kuhakikisha sauti zao zinapazwa na kusikilizwa

(SAUTI YA AMANY)

“Mosi msaada wa familia na huduma ya mapema kwa watoto wenye down syndrome ni muhimu sana katika kuwezesha ukuaji na maendeleo yao, pili mchangamano na wengine na shule za chekechea , pia kuwapa elimu maalumu ni jambo la tatu la muhimu kwa wagonjwa hao , kwani Sanaa na kazi za mikono huwasaidia kubaini ni maeneo gani ambayo wanayamudu na wanaweza kufanya vizuri wakajivunia, na mwisho elimu ya kuwalinda watoto wenye ugonjwa unaoathiri uwezo wa kuelewa, tunatumai nchi zote zitazingatia mambohaya.”