Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwakilishi wa wanawake kwenye serikali na bunge wadorora- IPU

Uwakilishi wa wanawake kwenye serikali na bunge wadorora- IPU

Idadi ya wanawake walioko kwenye serikali na mabunge kote duniani inadorora licha ya matumaini kuwepo mwaka 2015.

Hiyo ni kwa mujibu wa ramani mpya kuhusu wanawake katika siasa mwaka 2017 iliyozinduliwa hii leo jijini New York, Marekani na umoja wa mabunge duniani, IPU na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya wanawake, UNWomen kando mwa kikao cha kamisheni ya hali ya wanawake.

Mathalani idadi ya wanawake marais au wakuu wa serikali imeshuka kutoka 19 mwaka 2015 hadi 17 mwaka huu.

Hata hivyo idadi ya maspika wabunge wanawake imeongezeka ingawa katika kiwango kidogo wakati huu ambapo usawa wa kijinsia unapigiwa chepuo.

Idadi ya mawaziri wanawake nayo imepungua hasa barani Afrika ambapo wanawake mawaziri ni asilimia 19.7 huku Congo-Brazaville na Zambia zikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mawaziri wanawake.

Akizungumzia ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa IPU Martin Chungong amesema uwiano sawa katika uwakilishi kwenye nafasi za uongozi ni msingi katika kuwepo kwa demokrasia wajibishi.