Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa malipo sawa kwa wanaume na wanawake:UN Women

Ni wakati wa malipo sawa kwa wanaume na wanawake:UN Women

Patricia Arquette nyota wa Marekani wa kucheza filamu amekuwa miongoni mwa wanaharakati mashuhuri waliotoa wito katika kikao cha 61 ya kamisheni ya hali ya wanawake duniani wa kumaliza tofauti za kijinsia imataifa na kuziba pengo la malipo baina ya wanaume na wanawake. Kikao hicho kilichofunguliwa Jumatatu katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kitaendelea hadi Machi 24. Bi Arquette akiongoza mjadala huo amesema.

(CLIP YA PATRICIA)

“Kuna huu wizi wa asilimia 23 ya mishahara ya wanawake kote duniani , hivyo bado ni tatizo kubwa.Namaanisha ninapoangalia nchini mwangu , ninapoangalia Marekani , ndio kuna mikakati mingi ya kulinganisha malipo, lakini itatimizwa kweli. Kutakuwa na ari ya kushitaki, kuchukunguza kiwango hicho , hatujui .Na kuna mataifa mengi hususani yale ambayo wanawake wanalipiwa kidogo sana na pengo la kijinsia ni kubwa mno , hakuna watunga sheria wanaoweka sheria yoyote. Na kwa njia nyingi tunaona haki za wanawake zinarudishwa nyuma Marekani , hivyo ni wakati mgumu wa kuwa na uhakika, na nadhani ni muhimu sana kwa wanawake kuwa na usawa Marekani na duniani kote.”

Inakadiriwa kuwa kwa wastani wa kimataifa, wanawake wanalipwa senti 77 tu kwa kila dola moja ambayo wanaume hulipwa na matokeo yake wanawake zaidi wanastaafu katika umaskini kwa sababu ya maisha kutokuwa na usawa wa mapato kati yao na wanaume. Takwimu zinaonyeshsha kuwa kuna pengo la kimataifa la ujira kwa asilimia 23, na katika baadhi ya nchi nyingine pengo hilo ni kubwa zaidi, wanawake nchini Sweden na Ufaransa wanalipwa asilimia 31 chini kuliko wanaume, ambapo nchini Ujerumani ni asilimia 49 na asilimia 75 kwa wanawake nchini Uturuki.

Moja ya sababu kuu ya pengo hilo ni kwamba wanawake hufanya kazi mbalimbali kuliko wanaume, kama vile ualimu, huduma za afya, au huduma za kulea watoto na sekta zinazolipa kiwango chini.

Bi Arquette ambaye pia ni mwanachama wa shirika la usawa wa malipo na mwigizaji aliyepata tuzo ya Oscar akiungana na wanaharakati wengine mashuhuri akiwemo Abby Wambach mmarekani anayesakata kabumbu wameahidi kutoa mwangaza zaidi juu ya ubaguzi wa aina hii na kusaidia jitihada za kukomesha pengo la kijinsia katika malipo.

Naye mkurugenzi wa UN Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema mwenendo huu unaathiri kila nchi kote duniani na ni wakati wa kulivalia njuga suala hilo. Wengine waliopaza sauti zao ni mkurugenzi mkuu wa ILO Guy Ryder na Waziri wa Masuala ya Jamii na Usawa wa Iceland Bi Thorsteinn Víglundsson, waliokuwa miongoni ya wadhamini wa tukio hilo.