Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muenzini Maathai kwa kuhifadhi mazingira : UNEP

Muenzini Maathai kwa kuhifadhi mazingira : UNEP

Leo ni siku ya mazingira barani Afrika, siku ambayo pia imepewa heshima ya kuitwa siku ya Wangari Maathai,mwanaharakati wa mazingira kutoka Kenya ambaye enzi za uhai wake alipigia chepuo uhifadhi wa mazingira.

Kupitia wavuti wake hii leo, Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira UNEP, limezitaka nchi za Afrika kuainisha mafaniko katika uhifadhi wa mazingira ikiwa ni sehemu ya kumumezi mwanaharakati huyo.

Muungano wa Afrika AU, kupitia mkutano wake mjini Addis Ababa nchini Ethiopia miaka mitano iliyopita, uliamua kutambua rasmi maisha na kazi za marehemu Maathai, aliyekuwa balozi wa mazingira wa AU na mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

AU pia ilitangaza tuzo ya Wangari Maathai anayokabidiwa mtu au watu waliofanikiwa katika kuhifadhi mazingira na viumbe hai.