Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujerumani ni mfano wa kuvumiliana duniani:Guterres

Ujerumani ni mfano wa kuvumiliana duniani:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ambaye amekuwa ziarani nchini Ujerumani , hii leo akizungumza na wandishi wa habari mjini Munich pamoja na kansela wa nchi hiyo, Angela Merkel na kusema matatizo yakimataifa yanahitaji suluhu ya kimataifa, akiongeza kuwa kumekuwa na ongezeko la migogoro ulimwenguni, ambapo ile ya kale haijaisha na inazidi kuwa mbaya zaidi huku tishio jipya la ugaidi wa kimataifa likiibuka. Na hivyo akatoa wito wa mshikamano.

(Sauti ya Guterres)

"Matatizo ya kimataifa yanahitaji suluhisho la kimataifa. Mimi kweli naamini katika ushirikiano wa kimataifa, haja ya nchi kuja pamoja na kutumia taasisi za kimataifa na kuwa na uwezo na mshikamano, ili kukabili changamoto kubwa zinazoikumba dunia ya leo. Ujerumani ni nguzo imara sana ya taasisi zetu za kimataifa. Na ina jukumu muhimu sana katika mfumo wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na katika taasisi nyingi nyingine za kimataifa. Tayari Ujerumani imefanya kazi sana katika nyanja zote ambapo jumuiya ya kimataifa inahitajika kuja pamoja ili kukabiliana na changamoto kubwa ambayo ni tisho kwa  maisha yetu ya kila siku.

Bwana Guterres amemshukuru mwenyeji wake akisema Ujerumani imekuwa mfano katika masuala ya kuvumuliana duniani

(Sauti ya Guterres)

Serikali ya Ujerumani na kiongozi wake Angela Merkel wamekuwa ishara ya uvumilivu, ishara ya ukarimu kwa watu wanaohitaji ulinzi. Mfano ambao ningependa kuona unaigwa a na wengine katika sehemu nyingi nyingine za dunia ili tuweze kukabiliana na mateso makubwa ambayo yanashuhudiwa kwa sababu ya migogoro ya kutisha kote ulimwenguni.

Guterres amesema ushikamano una matatizo mengi duniani ambapo wengi wanakataa utofauti uliopo na kutoelewa kuwa utofauti ni utajiri na sio tishio.  Ameongeza kuwa ana hakika kwamba ushirikiano na serikali ya Ujerumani utakuwa imara kama chanya na mafanikio kama wakati alipokuwa kamishna mkuu wa kuhudumia wakimbizi.