Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watoto milioni nne kunufaika na chanjo dhidi ya Surua.

Zaidi ya watoto milioni nne kunufaika na chanjo dhidi ya Surua.

Kampeni kubwa ya utolewaji wa chanjo dhidi ya surua nchini Nigeria inatarajiwa kuanza hapo kesho, ambapo watoto zaidi ya milioni nne katika maeneo yenye mizozo Kaskazini Mashariki watanufaika, limesema Shirika la afya ulimwenguni WHO.

Katika taarifa yake, WHO imesema chanjo hiyo katika majimbo ya ya Borno, Yobe na Adamawa ambayo yameathiriwa na machafuko yatokanayo na kundi la kigaidi la Boko Haram, inawalenga watoto walio kati ya umri wa miezi sita hadi miaka 10.

Shirika hilo limesema kwamba chanjo hiyo ni muhimu hasa kwa kuzingatia kuwa machafuko yametatiza mifumo ya afya nchini Nigeria kwa miaka mingi, na kuathiri upatikanaji wa chanjo kwa watoto.

Katika kufanikisha kampeni hiyo,WHO inasaida mashirika ya afya katika majimbo hayo matatu, huku ikifanya kazi kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, na kituo cha Marekani cha udhibiti wa magonjwa CDC.