Guterres apendekeza kikosi kazi kukabiliana na ukatili wa kingono

Guterres apendekeza kikosi kazi kukabiliana na ukatili wa kingono

Kupitia mashauriano na wajumbe wa kamati tendaji aliyoiunda, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemuagiza mratibu maalum wa kuboresha mwenendo wa Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na masuala ya unyanyasaji na ukatili wa kingono Bi Jane Holl Lute kuunda kikosi kazi cha ngazi ya juu kuhusu suala hilo.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imesema kikosi kazi hicho kina wajibu wa kutekeleza kwa haraka , kwa uwazi mkakati wa hatua yakinifu na wajibishi za Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na kuzuia unyanyasaji na ukatili wa kingono

Kikosi kazi hicho chenye wajumbe tisa wakiwamo Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kimataifa la uhamiaji William L. Swing, na Msaidizi wa Katibu Mkuu katika idara ya usaidizi kwenye maeneo ya Umoja wa Mataifa unapofanya kazi.

Yumo kadhalika Mkuu wa wafanyakazi katika ofisi ya mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono kwenye maeneo yenye vita, Bi Nancee Bright.

Taarifa hiyo imesema kuwa kikosi kazi hicho kitatumia ripoti ijayo ya Katibu Mkuu kuhusu hatua za ulinzi dhidi ya unyanyasaji wa kingono kuwasilisha muundo wa mkakati na kuongeza kuwa Mwenyekiti wake atawajibika kuwasiliana na wadau wakiwamo nchi wanachama, wadau wengine nje ya Umoja wa Mataifa na mashirika husika.