Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu launda chombo kuchagiza uchunguzi wa haki Syria

Baraza Kuu launda chombo kuchagiza uchunguzi wa haki Syria

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalounda utaratibu wa kusaidia kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo uhalifu wa kivita tangu kuanza kwa mzozo nchini Syria mwaka 2011. Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 105 nchi 15 zikipinga ilihali 52 hazikupiga kura.

Chombo hicho kitashirikiana na tume huru ya uchunguzi ya kimataifa kuhusu Syria iliyoundwa mwaka 2011 na Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa. Catherine Pollard ni mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa inayotoa usaidizi kwa Baraza Kuu.

(Sauti ya Catherine)

"Baraza Kuu litaamua kuanzisha chombo cha kimataifa, huru na kisichoegemea upande wowote kusaidia uchunguzi wa wale wote wanaowajibika na uhalifu mkubwa zaidi wa kijinai huko Syria kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Chombo kitakuwa chini ya Umoja wa Mataifa na kitashirikiana kwa karibu na tume huru ya kimataifa ya uchunguzi Syria katika kukusanya, kuweka pamoja, kuhifadhi na kuchambua matukio ya ukiukwaji wa sheria za haki za binadamu na ukatili"

Amesema chombo hicho kitaandaa makabrasha ili kuwezesha mchakato wa haraka wa keshi kwa mujibu wa sheria za kimataifa kwenye mahakama za kimataifa, kitaifa au kikanda ambazo tayari zina mamlaka au zitakuwa na mamlaka za kuendesha kesi hizo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.