Amina J Mohammed wa Nigeria ateuliwa Naibu Katibu Mkuu wa UM
Katibu Mkuu mteule wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amefanya uteuzi wa maafisa watatu waandamizi zaidi kwenye umoja huo ikiwemo Naibu Katibu Mkuu ambaye ni Amina J Mohammed wa Nigeria.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ametaja maafisa wengine waandamizi walioteuliwa kuwa ni Maria Luiza Ribeiro Viotti wa Brazil ambaye anakuwa afisa mkuu mwandamizi au Chef de Cabinet huku Bwana Guterres akinukuliwa akieleza nia yake ya kuanzisha nafasi ya mshauri mkuu wa sera na kumteua Kyung-wha Kang wa Korea Kusini kushika wadhifa huo.
Kuhusu uteuzi huo wa wanawake watatu kushika nyadhifa hizo za juu zaidi kwenye Umoja wa Mataifa, Bwana Dujarric amemnukuu Katibu Mkuu mteule Guterres akisema..
(Sauti ya Dujarric)
“Nina furaha kutegemea jitihada kubwa za wanawake hawa watatu wenye ujuzi wa hali ya juu ambao nimewachagua kwa kuzingatia ubobezi wao kwenye masuala ya kimataifa, maendeleo, diplomasia, haki za binadamu na usaidizi wa kibinadamu.”

Bi. Amina Mohammed ambaye anakuwa mwanamke wa tatu kushika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwa sasa ni Waziri wa mazingira wa Nigeria ambapo anachochea jitihada za nchi yake kulinda mazingira na rasilimali kwa maendeleo endelevu.
Kabla ya wadhifa wa sasa alikuwa mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuhusu ajenda baada ya mwaka 2015 ambako alikuwa mstari wa mbele kwenye kuundwa kwa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.
Kwa upande wake Bi. Maria Luiza Ribeiro Viotti kwa sasa anahudumu nchini Brazili kwenye Wizara ya mambo ya nje akijikita kwenye nchi za BRICS ambazo ni Brazili, India, China na Afrika Kusini.
