Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto msipuuze mawazo yenu- Malala

Watoto msipuuze mawazo yenu- Malala

Malala Yousfzai, mwanaharakati na mtetezi wa elimu ya mtoto wa kike, ametangazwa rasmi kuwa mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa.

Uteuzi wa Malala ulitangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António  Guterres katika hafla iliyofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa alasiri ya tarehe 10 Aprili.

Nats..

Utangulizi wa Bwana Guterres ulisheheni sifa lukuki kwa Malala mwenye umri wa miaka 19 hivi sasa ambaye alinusurika kifo wakati wataliban nchini mwake Pakistani walipompiga risasi mwaka 2012.

image
Baba mzazi wa Malala (kushoto) akiwa na Naibu Katibu Mkuu wa UM Amina J Mohammed, wakifuatilia tukio la mwanae kutangazwa mjumbe wa amani wa UM. (Picha:UNVideo capture)
Bwana Guterres anasema kuwa Malala anakuwa balozi wa amani mdogo zaidi wa Umoja wa Mataifa na uteuzi huo umetokana na..

(Sauti ya Guterres)

“Kuhamasishwa na kujitoa kwako katika maadili ya Umoja wa Mataifa hasa dira yake ya maisha yenye utu kwa watu wote na kuvutiwa na utetezi wako wa kijasiri kwa haki za watu wote hasa elimu na usawa kwa wanawake na wasichana.”

image
Hadhira wakati wa tukio la Katibu Mkuu wa UM António Guterres kutamgaza Malala kuwa mjumbe wa amani wa UM kwenye makao makuu ya UM, New York, Marekani. (picha:UNVideo capture)
Malala akapatiwa fursa ya kuzungumza akianza kwa kushukuru mola na hatimaye kutoa wito kwa watoto wa kike..

(Sauti ya Malala)

“Nawahamasisha watoto wote wa kike mnapaswa msimame kidete, inabidi mjiamini. Ninyi ndio waleta mabadiliko halisi. Iwapo hamtasimama, mabadiliko hayatakuja.”

Muda wa maswali kutoka kwa wageni vijana ukawadia ambapo baadhi walisaka ushauri kutoka kwa Malala juu ya kile wanapaswa kufanya….

image
Malala Yousfzai akimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa UM Antonio Guterres wakati akisomewa majukumu yake ya ujumbe wa amani wa Umoja huo. (Picha:UNvideo capture)
(Sauti ya Malala)

“Huwa najiambia kila wakati jiamini. Amini mawazo yako. Mara nyingi tunadhani kuwa tu watoto na mawazo yetu hayako kwenye kiwango cha kutekelezwa. Mawazo na fikra zenu ni muhimu na yaaminini. Yapo mara nyingi mawazo ya watu wazima na hayatekelezeni. Tunashuhudia kote duniani.”

Alipoulizwa ni kwa jinsi gani baba yake amechangia fursa alizo nazo sasa? Malala alieleza kuwa baba yake alimuunga mkono kila hatua aliyopitia na hivyo amesema..

(Sauti ya Malala)

“Wanaume hawapaswi kukata mabawa ya wanawake na badala yake waacheni waruke na wasonge mbele.”

Malala amesema kuwa ingawa kwenye bonde la Swat alikokuwa anaishi mazingira yalikuwa magumu, aliamua kujitoa kimasomaso kuokoa watoto wengine jambo ambalo Katibu Mkuu Guterres amesema ni jambo la kipekee la mtu kusimamia ukweli licha ya kufahamu kuwa utagharimu uhai wake.