Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na Uganda watia shime ukomeshwaji wa machafuko Sudan Kusini

UM na Uganda watia shime ukomeshwaji wa machafuko Sudan Kusini

Wakati idadi ya watu waliokimbilia Uganda kutoka Sudan Kusini tangu Julai mwaka huu imefikia zaidi ya 300,000, mashirika sita ya Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uganda, wanataka jumuiya ya kimataifa kufanya kila juhudi ili kutia ukomo mzozo wa Sudan Kusini unaosababisha mateso kwa raia wasio na hatia. Taarifa Kamili na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Serikali na mashirika hayo yakiwemo lile la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), shirika la Uhamiaji (IOM),shirika la Mpango wa Chakula (WFP) na lile la kuhudumia watoto (UNICEF), wamesema katika taarifa ya pamoja kuwa, ingawa ni muhimu kuendeleza ushirikiano ili kufikia mahitaji ya kuokoa maisha ya wakimbizi hao, ni vyema kutafuta suluhu la kudumu kwa mzozo wa Sudani Kusini.

Wamesema ni lazima mateso dhidi ya raia wa nchi hiyo yanayowalazimisha kukubali kugeuka wakimbizi yakomeshwe.

Ripoti ya wakimbizi inasema, vikundi vilivyojihami hasa katika maeneo ya Euatoria vinaendelea kushambulia vijiji vikiuauwa wananchi, kuchoma moto nyumba zao, kubaka wanawake na wasichana na mara nyingine kuteka vwanaume na wavulana.

Tangu kuvunjika kwa usalama Sudani Kusini mwaka 2013, watu zaidi ya nusu milioni wamekimbilia Uganda, nchi inayohifahdi wakimbizi takriban milioni moja.