Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jeshi ondokeni katika jengo la tume ya uchaguzi Gambia: Ban

Jeshi ondokeni katika jengo la tume ya uchaguzi Gambia: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amefedheheshwa na hatua ya jengo la tume huru ya uchaguzi nchini Gambia IEC, kuwekwa chini ya ulinzi wa jeshi la nchi hiyo.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imemnukuu akilaani hatua hiyo aliyoiita ya kusikitisha na ukosefu wa heshima kwa matakwa ya watu wa Gambia na jumuiya ya kimataifa wakati huu ambapo ujumbe wa ngazi ya juu ya jumuiya ya uchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS, ilikuwa nchini humo kufanikisha kukabidhi madaraka kwa amani.

Ban amesema kitendo hicho kinakiuka uhuru wa IEC, chini ya katiba ya Gambia na inaweza kuharibu malighafi muhimu za tume hiyo.

Amesisitiza wito wake wa makabidhiano ya madaraka kwa amani, wakati na utaratibu, kwa kuheshimu matakwa ya watu wa Gambia ambayo yalidhirishwa wakati wa uchaguzi. Amelitaka pia jeshi la nchi hiyo kuondoka katika jengo la tume ya uchaguzi, na kujizuia na vitendo vyovyote vinavyozuai juhudi za kukabidhi madaraka kwa amani.

Katibu Mkuu Ban pia ametaka wale wote watakaobainika kusababisha machafuko na ukatili dhidi ya haki za binadamu kuwajibishwa.