Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cameroon yapatiwa dola milioni 325 kuimarisha mtandao wa umeme

Cameroon yapatiwa dola milioni 325 kuimarisha mtandao wa umeme

Benki ya dunia imeidhinisha mkopo wa dola milioni 325 kwa ajili ya kuimarisha ubora wa mtandao wa umeme nchini Cameroon.

Mkurugenzi wa Benki ya dunia nchini humo Elisabeth Huybens amesema mkopo huo utasaidia harakati za Cameroon za kuboresha huduma na usambazaji wa umeme na kufungua fursa za uwekezaji wa sekta binafsi.

Halikadhalika utasaidia kampuni mpya ya umeme ya taifa, SONATREL ili iweze kufanya kazi yake kwa ukamilifu hasa katika miaka yake hii ya mwanzo ya utendaji.

Bi. Huybens amesema ikiwa ni asilimia 74 tu ya wananchi wa Cameroon wanaoishi vitongojini ndio wanapata umeme, huduma bora ni muhimu wakati huu ambapo inaelezwa kuwa ukosefu wa umeme ni kikwazo cha ukuaji wa uchumi.

Hii ni mara ya pili tangu mwaka 1992, Benki ya dunia kupitia taasisi yake ya IBRD inasaidia mradi wa marekebisho ya mfumo wa umeme nchini Cameroon.