Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Baraza la Usalama lataka majadiliano zaidi kufikia muafaka

DRC: Baraza la Usalama lataka majadiliano zaidi kufikia muafaka

barazadrc

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wanaozuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC tangu Novemba 11 wamesema makubaliano ya kisiasa yaliyotiwa saini mwishoni mwa mazungumzo ya kitaifa hivi karibuni ilikuwa hatua muhimu, lakini  wanataka kuendelea kwa majadiliano Zaidi ili kufikia muafaka wenye wigo mpana zaidi.

Wajumbe hao wametoa wito kwa wadau wa kisiasa na kijamii kuchukua jukumu zaidi kuhakikisha wanafikia muafaka wa tarehe ya uchaguzi unaojumuisha wote , pia limetoa wito wa kuondoa marufuku ya maandano iliyowekwa hivi karibuni

Akizungumza baada ya mkutano wa saa karibu mbili kati ya ujumbe wa baraza hilo na Rais Joseph Kabila, balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, François Delattre amesema

(SAUTI BALOZI FRANCOIS)

“Makubaliano ya Oktoba 18 ni hatua. Majadiliano yanapaswa kuwa na uwezo wa kuendelea katika mfumo mmoja jumuishi ili kufikia makubaliano yenye wigo mpana zaidi kuhusu tarehe ya uchaguzi sanjari na hatua za kujenga Imani.Kwa mantiki hii nasisitiza kwamba uhuru wa maoni na kukusanyika lazima uhakikishwe na pia fursa sawa kwa vyombo vya habari ili kuwa na mjada wa kisiasa ulio muhimu na wa uhuru. Usalama na uhuru wa kutembea kwa wote lazima udumishwe, na kjwa hilo tunatoa wito kwa serikali ya Congo kurejesha hewani matangazo ya idhaa ya kimataifa ya Ufaransa RFI na kuondoa marufuku ya maandamano.”

image
Wajumbe wa baraza la Usalama nchini DRC. Picha na Radio Okapi:Jon Bompengo
Ujumbe wa baraza hilo pia umekuwa ukihofia hali ya usalama Mashariki mwa Congo, na kesho Jumapili utaelekea mjini Ben kwa mara ya kwanza . Balozi wa Angola kwenye Umoja wa Mataifa Ismael Abraao Gaspar pia amesema kuwa makubaliano kutokana na mazungumzo Muungano wa Afrika yalikuwa msingi unaopaswa kuendelea na ni lazima kuhakikisha uchaguzi wa kuaminika na kuepuka machafuko nchini humo.

(SAUTI BALOZI GASPAR)

"Mkakati upo, na utekelezaji utaanza na hilo limetupa hakikisho zaidi. Makubaliano yaliyotoiwa saini ni msingi mzuri ambao ni lazima ujengwe. Na nani wa kuujenga? Ni watu wa Congo na viongozi wao na watu wote. Lakini kujenga sio kuharibu , kujenga maana yake sio kupandikiza ghasia katika nchi hiyo ambayo haiwezi kuendelea kuishi katika hali ya zamani. Ni lazima tusonge mbele kuelekea kwenye uchaguzi , tuelekee kwenye ujenzi wa taifa hili.”

Ujumbe huo ambao utakuwa DRC kwa siku tatu utaelekea Luanda Angola ambako utakuwa na mazungumzo na Rais wan chi hiyo, bunge na asasi za kiraia.