Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN Women na UNICEF wasisitiza umuhimu wa takwimu kwa maendeleo ya wasichana Iraq:

UN Women na UNICEF wasisitiza umuhimu wa takwimu kwa maendeleo ya wasichana Iraq:

Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na masuala ya wanawake UN Women na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wamesema wanatambua hatua zilizopigwa kote duniani katika kuchagiza haki za mtoto wa kike lakini pia wanataka kutanabaisha changamoto zilizopo zinazohitaji kushughulikiwa.

Wamesema nchini Iraq wasichana wamekuwa wahanga wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwepo kutekwa, kusafirishwa kiharamu, mateso, ndoa za utotoni , utumwa wa ngono na mifumo mingine ya ukatili wa kijinsia.

Wasichana milioni 3.5 nchini humo hawaendi shule na ndio idadi kubwa ya watoto wasiokwenda shule. Mashirika hayo yameongeza kuwa wasicha 975,000 nchini Iraq wameolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 15 ikiwa ni mara mbili ya idadi ya 1990, na bila ya twakimu idadi hiyo isingejulikana.

Wamesisitiza kuwa kitu muhimu kwa maendeleo ya wasichana ni kukusanya takwimu zinazoelezea changamoto zinazowakabili, mafanikio na maeneo ya kuboresha.